Iran yajibu madai mapya ya Marekani; Washington haina haki ya kusema chochote
Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI) amepinga madai mapya ya Marekani kuhusu ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kusisitiza kuwa, nchi ambazo zimeshindwa hata kulaani vitendo vya kigaidi vilivyofanywa katika taasisi za nyuklia za Iran, hazina haki ya kusema chochote kuhusu miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.
Bw. Mohammad Eslami amewaambia waandishi wa habari mjini Moswoe kwamba Russia ni mwanachama wa kundi la 4+1 la mapatano ya nyuklia ya JCPOA, na leo Iran inazungumza nayo kuhusu mradi wake wa amani wa nyuklia.
Bw. Eslami ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili mjini Moscow leo Jumanne akiongoza ujumbe wa Iran kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mkuu mwenzake wa taasisi ya nyuklia ya Russia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda wote imekuwa ikisisitiza kuwa, miradi yake ya nyuklia ni ya amani kikamilifu na hilo limethibitishwa katika ripoti chungu nzima za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA.
Vile vile Iran inasema kuwa, imeruhusu wakaguzi wa kimataifa kukagua maeneo yote yaliyokubaliwa katika mapatano ya pande mbili na haijawahi kuzuia ukaguzi wowote unaofuata sheria na makubaliano yaliyofikiwa.
Akiwa ziarani mjini Moscow, Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI) atajadiliana na wenzake wa Russia masuala mbalimbali yanayohusiana na miradi ya nyuklia pamoja na namna ya kuimarishwa zaidi na zaidi ushirikiano wa pande mbili.