Iran: Inachofanya Israel ni kuhatarisha usalama wa Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i75326-iran_inachofanya_israel_ni_kuhatarisha_usalama_wa_asia_magharibi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Bunge amesema kuwa, Wazayuni wanachochea kwa makusudi machafuko ili kuhatarisha usalama wa eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2026-08-11T03:40:48+00:00 )
Oct 03, 2021 01:09 UTC
  • Iran: Inachofanya Israel ni kuhatarisha usalama wa Asia Magharibi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Bunge amesema kuwa, Wazayuni wanachochea kwa makusudi machafuko ili kuhatarisha usalama wa eneo la Asia Magharibi.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Sayyid Mohammad Hosseini akisema hayo na kuongeza kuwa, wanachofanya Wazayuni ni kuchochea vurugu katika eneo hili zima ikiwa ni pamoja na kuzichochea Jamhuri ya Azerbaijan na eneo la Kurdistan la Iraq kuharibu utulivu na usalama wa eneo la kaskazini mwa Asia Magharibi.

Amesisitiza kuwa, dunia inapaswa kutambua kuwa usalama wa eneo hili ni mstari mwekundu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba Tehran haiwezi kunyamazia kimya njama zozote za kuhatarisha usalama huo.

Bendera ya utawala wa Kizayuni

 

Makamu wa Rais wa Iran amesema, luteka na mazoezi ya kijeshi ya "Wakombozi wa Khaibar" yamefanywa na Jamhuri ya Kiislamu kwa lengo la kujiwekea kinga na kuwa tayari kuilinda mipaka yake iwapo kutatokezea shambulio lolote lile.

Ameongeza kuwa, baadhi ya nchi za eneo hili zinapenda kujitanua na zinajifanya hazielewei kuwa, mipaka ya Mapinduzi ya Kiislamu imefika hadi katikati ya Ulaya.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Bunge vile vile amegusia nguvu za kieneo za Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, Marekani imejileta yenyewe Asia Magharibi na hivi sasa imezama kwenye kinamasi huko Iraq. Lakini pia imelazimika kukimbia Afghanistan baada ya miaka 20 ya kufeli kwake mtawalia.