Iran yaitaka IAEA itangaze msimamo wake kuhusu ugaidi wa Israel
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomi ya Iran (AEOI) ameutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA utangaze msimamo wake kuhusu vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Mohammad Eslami akisema hayo jana baada ya kikao cha pamoja na wajumbe wa kamati ya kifungu cha 90 cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran na kusema kuwa, wakala wa IAEA unapaswa kutangaza msimamo wake kuhusu matukio ya kigaidi dhidi ya taasisi na mradi wa nyuklia wa Iran ambayo utawala wa Kizayuni umetangaza wazi kuwa ndio uliohusika.
Siku chache zilizopita pia, Mkuu huyo wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI) alisema kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) ambao ni jumuiya huru na ya kimataifa haupasi kuwa uwanja wa michezo wa magenge ya kigaidi.
Mohammad Eslami ambaye alikuwa akizungumza na shirika la habari la Sputnik kuhusu misimamo ya karibuni ya wakala wa IAEA dhidi ya mradi wa kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran amesema kuwa, ugaidi wa kinyuklia umekuwa ukitoa tuhuma dhidi ya Iran kwa kutegemeza njama za makaratasi na picha za satalaiti zisizo na msingi wowote. Amesisitiza kuwa mbinu hiyo imechakaa na kupitwa na wakakati.
Hivi karibuni pia Bw. Mohammad Eslami alipinga madai ya Marekani kuhusu ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kusisitiza kuwa, nchi ambazo zimeshindwa hata kulaani vitendo vya kigaidi vilivyofanywa katika taasisi za nyuklia za Iran, hazina haki ya kusema chochote kuhusu miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.