Amir-Abdollahian: Makubaliano mazuri ya JCPOA yanaweza kufikiwa ndani ya muda mfupi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: ikiwa Marekani na nchi tatu za Ulaya zitakuwa na nia ya dhati kuhusiana na kurejea kwenye utekelezaji kamili wa majukumu yao yaliyoainishwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, mapatano yanaweza kufikiwa ndani ya muda mfupi.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran aliofanya pamoja na waziri mwenzake wa Ireland na akaongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kufikia makubaliano mazuri katika JCPOA.
Pamoja na hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, badala ya pande za Magharibi kucheza na matini ya makubaliano na badala ya kucheza na wakati na kupoteza muda inapasa zionyeshe irada na azma ya kweli ya kurejea kwenye utekelezaji kamili wa JCPOA.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, katika jumbe inazotuma kwa Jamhuri ya Kiislamu kupitia nchi zingine na pande unganishi, Marekani inazungumza lugha ya kuwa na nia njema ya kuifikia mapatano, lakini hadi wakati huu hakijafanyika chochote cha maana cha kuakisi na kubainisha kivitendo nia njema inayodai kuwa nayo Marekani.
Duru ya nane ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo ilianza mjini Vienna tarehe 27 Desemba; na baada ya kusitishwa kwa kipindi kifupi ili pande husika ziende kufanya mashauriano katika miji yao mikuu, ilianza tena tarehe 8 ya mwezi huu wa Februari, katika mji mkuu huo wa Austria.
Kwa kuzingatia ukiukaji makubaliano ya JCPOA uliofanywa na Marekani tangu siku za awali za utekelezaji wa mapatano wakati wa urais wa Barack Obama, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza katika duru zilizopita za mazungumzo ya sasa ya Vienna kuhusu ulazima wa kuwepo "hakikisho la kudumu makubaliano" na "uthibitisho wa kuondolewa vikwazo", yakiwa ndio matakwa yake mawili makuu ya kutekeleza tena kikamilifu makubaliano ya JCPOA.../