Abdollahian: Azimio la IAEA dhidi ya Iran lilichochewa kisiasa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezikosoa vikali Marekani na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kwa kuwasilisha azimio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu mbele ya Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, hatua hiyo iliharakishwa na kupasishwa kwa malengo ya kisiasa.
Azimio hilo lilipendekezwa na Marekani pamoja na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na lilipasishwa Jumatano iliyopita na Bodi ya Magavana ya IAEA licha ya upinzani mkali wa China na Russia.
Mbali na kujadili kuhusu mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, Austria, Amir-Abdollahian na Guterres wamegusia masuala ya kieneo na kimataifa, hususan mgogoro wa Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kuunga mkono usitishaji vita nchini Yemen, na inataka kuondolewa kikamilifu mzingiro dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu, na pia kuandaliwa mazingira ya kufanyika mazungumzo zaidi baina ya makundi ya Wayemen wenyewe.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ametaja hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendeleza harakati za kijeshi ndani ya ardhi ya Syria na kushambulia uwanja wa ndege wa kiraia mjini Damascus kama ukiukaji wa Hati ya Umoja wa Mataifa.
Amesema matukio ya eneo hili la Asia Magharibi yamethibitisha kuwa, vitendo viovu vya utawala haramu wa Israel dhidi ya usalama na uthabiti wa mataifa ya eneo hili bila shaka vitagonga mwamba.
Kwa upande wake, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema azimio la IAEA halikuwa na la ziada isipokuwa mapendekezo tu, huku akisisitizia haja ya kuendelezwa mazungumzo ya Vienna ya kuondolewa vikwazo Iran.
Aidha amepongeza jitihada za Iran na misimamo yake ya kuunga mkono usitishaji vita nchini Yemen na kuongeza kuwa, vikao vya Astana kuhusu amani ya Yemen ni jukwaa zuri la kujadili migogoro ya nchi hiyo maskini, na mvutano baina ya Syria na Uturuki.