Iran yalaani hujuma ya kigaidi iliyoua makumi msikitini Kabul
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililopelekea kuuawa makumi ya watu katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Katika taarifa jana Alkhamisi, Nasser Kanaani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani hujuma hiyo iliyolenga waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Swala katika msikiti mmoja ulioko Khair Khana, viungani mwa Kabul.
Amesema: Iran inatoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Afghanistan kutokana na shambulio hilo la kikatili lililofanywa na magaidi wasio na chembe ya utu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametaka hatua zichukuliwe za kukomeshwa kabisa vitendo hivyo vya kigaidi si tu katika nchi hiyo na eneo la Asia Magharibi, bali kote duniani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo la Jumatano usiku imeongezeka na kufikia watu 21. Aidha makumi ya waumini waliokuwa katika msikiti huo wamejeruhiwa.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lakini weledi wa mambo wanaamini kuwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ndilo lililohusika.
Mapema mwezi huu, kundi hilo la kigaidi lilikiri kuhusika na mlipuko mwingine uliotokea huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, ambao ulipelekea watu 8 kuuawa shahidi na wengine 18 kujeruhiwa.