Rais Ebarahim Raisi: Iran ni tumaini la wanyonge na majuto kwa mabeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i87324-rais_ebarahim_raisi_iran_ni_tumaini_la_wanyonge_na_majuto_kwa_mabeberu
Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, licha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya kila upande kwa makumi ya miaka sasa, lakini vijana wa nchi hii wakiwemo wa sekta ya ulinzi wamepiga hatua kubwa ya kujivunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2022 20:55 UTC
  • Rais Ebarahim Raisi: Iran ni tumaini la wanyonge na majuto kwa mabeberu

Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, licha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya kila upande kwa makumi ya miaka sasa, lakini vijana wa nchi hii wakiwemo wa sekta ya ulinzi wamepiga hatua kubwa ya kujivunia.

Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana kwenye kikao na wakuu na wafanyakazi wa Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimizo ya tarehe 31 Mordad (kwa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia) ambayo ni Siku ya Viwanda vya Ulinzi nchini Iran. 

Vile vile amesema maendeleo makubwa waliyopata wanasayansi, wasomi na watu wenye vipaji maalumu nchini Iran katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda vya ulinzi si kwa manufaa ya Iran tu, bali yanaleta matumaini mema kwa Ulimwengu wa Kiislamu, kwa wanyonge na wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kama ambavyo yanaleta majuto pia kwa ulimwengu wa kufru.

Kijiji cha makombora nchini Iran yanayosubiri kukabiliana na ubeberu wa maadui

 

Amegusia sifa tatu kuu za zana zinazozalishwa kwenye viwanda vya ulinzi vya Iran ambazo ni umakini wake wa hali ya juu, athari zake kubwa na kujiendesha zenyewe silaha hizo na kusisitiza kuwa, leo hii Jamhuri ya Kiislamu ina nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote huku maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wakiwa hivi sasa ni dhaifu zaidi kuliko wakati wowote uliopita. 

Rais Ebrahim Raisi pia amesema, kilicholifanya taifa la Iran kuwa na ushawiwishi katika eneo hili na duniani kiujumla, ni kuwa kwake na nguvu kazi ya maana, vijana wanamapinduzi na mafanikio ya wasomi na wanasayansi wake hasa katika sekta ya ulinzi.

Pia amesema, maadui watambue kuwa, Iran ina nia ya kweli ya kuzidi kujiimarisha kimaendeleo katika nyuga zote na waelewe kuwa mikono ya mabeberu itakatwa kwenye eneo hili.