Kuundwa serikali ya wote, msimamo wa kiistratijia wa Iran kuhusu Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i87446-kuundwa_serikali_ya_wote_msimamo_wa_kiistratijia_wa_iran_kuhusu_afghanistan
Mwaka mzima umepita tangu kuingia tena madarakani kundi la Taliban nchini Afghanistan, lakini hadi hizi sasa kundi hilo halijatambuliwa kimataifa kutokana na misimamo yake.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 26, 2022 07:36 UTC
  • Kuundwa serikali ya wote, msimamo wa kiistratijia wa Iran kuhusu Afghanistan

Mwaka mzima umepita tangu kuingia tena madarakani kundi la Taliban nchini Afghanistan, lakini hadi hizi sasa kundi hilo halijatambuliwa kimataifa kutokana na misimamo yake.

Kundi la Taliban liliingia tena madarakani mwezi Agosti 2021 na liliahidi kuwa litaundwa serikali itakayokuwa na wawakilishi kutoka makundi na kaumu zote nchini humo, lakini haijatekeleza ahadi hizo hadi hii leo.

Mwaka mzima umepita na kundi hilo halioneshi hamu yoyote ya kuunda serikali inayoshirikisha watu wa makundi na mbari zote za nchi hiyo ijapokuwa hilo ni moja ya masharti makuu ya jamii ya kimataifa ya kuitambua serikali ya kundi hilo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo katika kipindi cha miongo kadhaa imebeba mzigo mkubwa wa kuwahudumia raia wa Afghanistan kutokana na kukosekana utulivu na kuendelea vita katika nchi jirani ya Afghanistan, muda wote imekuwa ikitilia mkazo wajibu wa kuchungwa na kudhaminiwa manufaa ya wananchi wa nchi hiyo. Hata baada ya kuanza utawala wa hivi sasa wa kundi la Taliban huko Afghanistan pia, msimamo mkuu wa Tehran ni kuundwa serikali ya wote nchini humo ili kuweza kuitoa Afghanistan katika migogoro mingi ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ambayo imedumu kwa makumi ya miaka ya vita na mapigano.

Hali ya kimaisha ni mbaya sana kwa wananchi wa Afghanistan

 

Kwa kweli unapoyaangalia matamshi ya msemaji wa kundi la Taliban, Zabiullah Mujahid, katika mazungumzo yake ya kwanza kabisa na waandishi wa habari baada ya kupinduliwa serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani na kuingia tena madarakani kundi hilo huko Afghanistan utaona kuwa, Taliban hawajatekeleza ahadi zao hata moja zilizotangazwa na Mujahid wakati huo, bali baadhi ya wakati kundi hilo hata linakwenda kinyume na ahadi zake.

Kundi la Taliban liliwaahidi wananchi wa Afghanistan kuwa litawaletea maisha mazuri, lakini mwaka mzima umepita na ndio kwanza maisha ya wananchi wa Afghanistan yanazidi kuwa magumu siku baada ya siku. Mfumuko wa bei umepanda vibaya nchini Afghanistan. Ughali wa maisha ni mkubwa kiasi kwamba mashirika ya misaada ya kibinadamu yametabiri kutokea mgogoro mkubwa wa kibinadamu kutokana na ukame pamoja na njaa kwa mamilioni ya Waafghani.

Kundi la Taliban liliwaahidi pia wananchi wa Afghanistan kuwaimarishia usalama wao jambo ambalo ni la kimsingi kabisa kwa kila jamii, hususan jamii za wachache. Lakini mwaka mzima umepita na si tu usalama ni mdogo bali wigo wa vitisho vya kiusalama nao umezidi kuwa mpana hususan dhidi ya watu wa dini na kaumu za watu wachache.

Viongozi wa kundi la Taliban la Afghanistan

 

Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndio maana mtazamo wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran ukawa ni kwamba, kwa vile jamii ya Afghanistan ina muundo wa kipekee wa makabila, dini na madhehebu tofauti, jukumu la serikali ya nchi hiyo ni kuwakilishwa na watu wa jamii zote na ni kwa njia hiyo tu ndipo itaweza kweli kusimamia na kudhamini mahitaji ya wananchi wote. Iwapo hilo halitozingatiwa, ni wazi kuwa linaweza kuzua migogoro mingine na pia kuzidisha moto wa migogoro iliyopo hivi sasa.

Jamii ya kimataifa nayo imeshurutisha misaada yake na kurekebishwa misimamo ya kundi la Taliban ambalo linalalamikiwa sana kwa kuendesha siasa za kundi na jamii moja tu na kudharau haki na matakwa ya kaumu na makundi mengine. Kundi hilo pia linapaswa kuzingatia madhara zinayopata nchi jirani na Afghanistan kutokana na wimbi la wakimbizi, ukosefu wa usalama mipakani na matatizo mengine mengi. Hivyo jambo la busara ni kufuata ushauri huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayokuwa na wawakilishi kutoka kada na mbari zote za Afghanistan.

Jamii ya kimataifa nayo na hasa nchi za Magharibi pia zimekuwa zikilitilia mkazo suala la kuundwa serikali ya wote nchini Afghanistan. Nchi hizo zimelivalia njuga sana suala hilo hivi sasa na ambalo limekuwa likisisitiziwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu zamani kabisa. Bila ya shaka ni kwa njia hiyo tu ndipo kundi la Taliban litaweza kuvutia misaada ya kibinadamu na hatimaye kupatikana utulivu wa kisiasa, kimaisha na kiusalama katika kona mbalimbali za Afghanistan.