Abdollahian: Hatua za kuondolewa Iran vikwazo zipo katika mkondo sahihi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema mazungumzo ya uondoaji vikwazo haramu ilivyowekewa Iran yanaendelea vizuri, na kwamba hatua za kuondolewa vikwazo hivyo zipo katika mkondo sahihi.
Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana Jumatatu na kueleza kuwa: Hivi sasa tumefikia hatua ya maelewano juu ya maudhui tofauti, na hii itasaidia kufika haraka kwenye marhala ya mwisho ya kufikiwa makubaliano.
Amesema, "Tunahisi kuwa upande wa Marekani hivi sasa unafanya mabadilishano ya jumbe ukiwa na uelewa wa hali halisi ya mambo, kinyume na hapo awali."
Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, Iran itakubali tu mapatano ambayo hayakanyagi mistari myekundu ya taifa hili, na yenye dhamana kuwa Jamhuri ya Kiislamu itastafidi kiuchumi.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, Iran ina nia ya dhati ya kufikia makubaliano na haitaacha kufanya kila juhudi ili kuweza kufikia makubaliano mazuri, madhubuti na endelevu.
Hivi karibuni, jumbe za uwakilishi za Iran na Marekani zilibadilishana jumbe kati yazo pambizoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Iran inasisitiza kuwa, inafungamana na majukumu yake ili kufikiwa mapatano mazuri na imara; ambapo Iran tayari imetoa jibu kwa rasimu ya majumuisho ya mwisho.