Iran: Magharibi inalipiza kisasi kwa kuwaua kwa umati wagonjwa Wairani
Msemaji wa Serikali ya Iran amelaani vikwazo shadidi vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kueleza kuwa, "Wamagharibi wanalipiza kisasi dhidi ya Wairani, kwa kuanzisha kampeni ya mauji ya kimbari dhidi ya wagonjwa wa nchi hii."
Ali Bahadori Jahromi amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lugha ya Kifarsi na kubainisha kuwa, kufikia Machi mwaka ujao 2023, Wairani 220 wanaosumbuliwa na maradhi ya damu ya thalassemia, watakuwa wahanga wa vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hili.
Amesema wagonjwa 70 wa maradhi hayo ya damu walipoteza maisha hapa nchini mwaka 2018, wagonjwa 90 mwaka 2019, wengine 140 mwaka 2020, huku 180 wakiaga dunia kwa maradhi hayo mwaka jana.
Amefafanua kuwa, kwa kuzingatia mwenendo huo, Wairani 220 wanaosumbuliwa na ugonjwa huo wa damu wa thalassemia, watakuwa wahanga wa vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hili mwakani.
Jahromi ameeleza bayana kuwa, Marekani inashadidisha vikwazo dhidi ya Iran wakati huu ambapo Wairani wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kipepeo (EB) wakiwemo watoto wadogo, wanapitia maumivu makubwa kwa kukosa dawa kutokana 'ugaidi wa kimatibabu.'
Wamagharibi wameghadhabika mno baada ya njama zao za kutaka kutumia malalamiko juu ya kifo cha binti wa Kiirani Mahsa Amini kuchochea ghasia na fujo hapa nchini kugonga mwamba.
Wizara ya Fedha ya Marekani hivi karibuni iliiwekea Iran vikwazo vipya katikati ya mazungumzo ya nchi hiyo na pande husika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanayolenga kuondoa vikwazo vilivyo kinyume na sheria vya Washington dhidi ya Tehran.