Iran: Vikwazo vya EU havina maana, ghasia haziruhusiwi popote duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89402-iran_vikwazo_vya_eu_havina_maana_ghasia_haziruhusiwi_popote_duniani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema ghasia, fujo na kuharibu mali za umma ni mambo yasiyokubalika katika sehemu yoyote ile duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2022 00:13 UTC
  • Iran: Vikwazo vya EU havina maana, ghasia haziruhusiwi popote duniani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema ghasia, fujo na kuharibu mali za umma ni mambo yasiyokubalika katika sehemu yoyote ile duniani.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumatatu katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter na kusisitiza kuwa, vikwazo ilivyowekewa Iran na Umoja wa Ulaya kwa kisingizio cha ghasia hizo havina umuhimu wowote. 

Huku akikosoa misimamo ya kinafiki na kindumakuwili ya nchi za Magharibi kuhusiana na fujo zinazoshuhudiwa hapa nchini, mwandiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema: EU kwa mara nyingine wamegeukia chombo kisicho na athari cha vikwazo dhidi ya Wairani, na huku wakifanya mahesabu ghalati, wamechukua misimamo isiyo na maana kwa kutegemea rundiko la taarifa zisizo sahihi.

Jana Jumatatu, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ulaya walitangaza kuwawekea vikwazo shakhsia 11 wa Iran na taasisi nne za Kiirani, ikiwemo Polisi ya Maadili ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Maafisa usalama katika nchi za Magharibi wakikabiliana na wafanya fujo

Aidha jana Jumatatu, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alisema aghlabu ya nchi zilizo mstari wa mbele katika kuihujumu Iran katika suala la haki za binadamu zimetenda jinai nyingi dhidi ya Iran ikiwa ni pamoja na kuliwekea taifa hili vikwazo.

Alisema mbali na kuliwekea taifa la Iran vikwazo vya aina mbalimbali vikiwemo vikwazo vya dawa, nchi hizo za Magharibi pia zimeyapa hifadhi makundi ya kigaidi ambayo yamewekwa pia katika orodha yao wenyewe na magaidi. 

EU inadai kuwa, imetangaza vikwazo hivyo dhidi ya shakhsia na taasisi hizo za kulinda amani na usalama na kudumisha sheria za Iran eti kwa kukiuka haki za binadamu kwenye ghasia za fujo na machafuko yanayoshuhudiwa hapa nchini.