Iran yatangaza vikwazo dhidi ya shakhsia na taasisi ya Canada
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i90022-iran_yatangaza_vikwazo_dhidi_ya_shakhsia_na_taasisi_ya_canada
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa imeyaweka majina ya shakhsia na taasisi ya Canada kwenye orodha yake ya vikwazo, kwa kuunga mkono ugaidi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 03, 2022 11:49 UTC
  • Iran yatangaza vikwazo dhidi ya shakhsia na taasisi ya Canada

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa imeyaweka majina ya shakhsia na taasisi ya Canada kwenye orodha yake ya vikwazo, kwa kuunga mkono ugaidi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano kuwa, imewawekea vikwazo shakhsia wanane na taasisi moja ya Canada, kwa kuunga mkono kwa hali na mali harakati za kundi la kigaidi la MKO.

Taarifa ya wizara hiyo imewataja shakhsia hao kama Marco Mendicino, Mbunge na Waziri wa Usalama wa Umma wa Canada na mwenzake wa Ulinzi, Anita Anand. Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo Richard Wagner, Mkuu wa Majeshi, Wayne Donald Eyre, Eric Kenny, Kamanda wa Jeshi la Anga na mwenzake wa Jeshi la Majini, Angus Topshee, Kamishna wa Polisi, Brenda Lucki, na David Brown, Jaji aliyetoa uamuzi wa kuzuiliwa mali za Iran nchini Canada.

Kadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa imeliweka gazeti la Canada la The National Post kwenye orodha yake ya vikwazo.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewawekea vikwazo shakhsia na taasisi hiyo ya Canada kwa kueneza ghasia na fujo nchini Iran, kuchochea na kuhamasisha vitendo vya kigaidi, na kukabiliana na juhudi na harakati za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na ugaidi.

Kundi la MKO linaloungwa mkono na Wamagharibi

Vikwazo walivyowekewa shakhsia na taasisi hiyo ya Canada ni vya kuzuia utoaji viza na kuingia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuzuiliwa mali na milki zao katika eneo lililo chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzuiwa akaunti zao za benki katika mfumo wa fedha na benki wa Iran.

Kabla ya hapo, Iran iliwawekea vikwazo shakhsia na taasisi kadhaa za Marekani na Umoja wa Ulaya, kwa kuunga mkono ugaidi na kuchochea moto wa ghasia na fujo hapa nchini.