Jan 08, 2023 06:56 UTC

Leo tarehe 8 Januari ni siku ambayo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (Sepah) lilishambulia kwa makombora kambi ya jeshi la Marekani ya "Ain al-Asad" nchini Iraq, shambulio ambalo liliakisiwa sana na vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa.

Katika kujibu kitendo cha kigaidi cha serikali ya Marekani cha kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lililenga kambi ya Marekani ya "Ain al-Asad" katika mkoa wa Anbar nchini Iraq mnamo Januari 8, 2020 kwa makombora zaidi ya 10.

Katika operesheni hiyo, makombora 13 ya balestiki aina ya Fateh-313 na Qiyam yalivurumishwa kwenye kambi ya Ain al-Asad, ambayo kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, kamanda wa Kikosi cha Wanaanga cha Sepah yalilenga na kuharibu pakubwa vifaa na zana muhimu za jeshi la Marekani katika kambi hiyo.

Donald Trump, Rais wa Marekani wakati huo, alidai baada ya operesheni hiyo ya makombora kwamba shambulio hilo halikuua wala kumjeruhi yeyote katika kambi ya Ain al-Assad lakini Pentagon ikatangaza Februari mwaka huo huo kwamba Wanajeshi 109 wa Marekani walipata majeraha makubwa ya ubongo katika shambulio hilo.

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh

 

Katika siku za kwanza za shambulio hilo, kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani na pia baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya viliripoti juu ya hofu na woga mkubwa uliowapata wanajeshi wa Marekani katika kambi ya Ain al-Asad katika usiku wa kutekelezwa shambulio hilo la makombora ya Iran.

Picha ambazo CNN na vyombo vingine vya habari vilizionyesha kutoka Ain al-Assad zilidhihirisha wazi uharibifu mkubwa uliosababishwa na makombora ya Iran kwenye kambi hiyo ya Marekani.

Jenerali McKenzie, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani wakati huo, alikiri kwamba alikuwa hajawahi kuona shambulio kali kama hilo na kwamba makombora ya Sepah yalitua kwenye vichwa vya wanajeshi wa Marekani.

Kanali Timothy Garland, kamanda wa kambi ya Ain al-Asad wakati wa shambulio la makombora la Iran, alisema: "Kwa hakika hali ilikuwa ya kutisha sana, sijawahi kuona kitu kama hiki huko nyuma. Tulikuwa kwenye maficho ya chini ya ardhi. Kila mara kombora lilipopiga, mawimbi ya mlipuko yalitikisa maficho yote. Hatukujua kilichokuwa kinaendelea nje."