Rais Raisi: China inakaribisha juhudi za Iran za kujiunga na BRICS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94126-rais_raisi_china_inakaribisha_juhudi_za_iran_za_kujiunga_na_brics
Rais Ebrahim Raisi amesema China imekaribisha juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuwa mwanachama wa jumuiya ya BRICS, inayojumuisha nchi tano zinazoongoza kwa uchumi unaoinukia duniani.
(last modified 2026-04-26T10:08:53+00:00 )
Feb 16, 2023 08:03 UTC
  • Rais Raisi: China inakaribisha juhudi za Iran za kujiunga na BRICS

Rais Ebrahim Raisi amesema China imekaribisha juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuwa mwanachama wa jumuiya ya BRICS, inayojumuisha nchi tano zinazoongoza kwa uchumi unaoinukia duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili mjini Tehran leo baada ya kukamilisha ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini China, Seyyid Ebrahim Raisi amesema uanachama wa Tehran katika umoja huo utakuwa na matunda.
"Kulikuwa na mjadala kuhusu uanachama wa Iran katika BRICS, na tuliona hamu ya China ya (kuona Iran inapata) uanachama huu," amesema Rais Raisi.
Kundi la BRICS linajumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Uchumi wa nchi hizo tano unachangia zaidi ya 40% ya idadi ya watu wote duniani na karibu robo ya pato la taifa la dunia nzima.
Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari, Seyyid Ebrahim Raisi amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mchango athirifu katika uga wa usalama kwenye ukanda huu na ulimwenguni kote na inapasa iwe na nafasi athirifu pia katika uchumi na biashara.
Rais Ebrahim Raisi akilakiwa na Rais Xi Jinping mjini Beijing

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kueleza kuwa uhusiano mzuri wa Iran na China, ambayo ni nchi yenye uchumi unaoinukia duniani ikiwa na nafasi kuu katika bara la Asia, unaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwa Tehran katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Akiashiria ziara yake aliyoielezea kuwa "yenye matunda na mafanikio makubwa sana" nchini China, Rais Raisi ameeleza matumaini yake kuwa Tehran na Beijing zitashuhudia kuboreshwa zaidi ushirikiano katika nyanja mbalimbali hususan katika biashara na uchumi.
Iran na China zilitia saini makubaliano ya kihistoria ya ushirikiano wa kimkakati wa miaka 25 mwezi Machi mwaka jana katika hatua ya kupinga na kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi hizo mbili vilivyowekwa na Marekani.../