Iran kuanza kuuza bidhaa za nyuklia nje ya nchi
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ametangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inajiandaa kuanza kusafirisha nje ya nchi bidhaa zake za nyuklia, zikiwemo za tiba.
Kwa mujibu shirika la habari la IRNA, Mohammed Eslami, Mkuu wa AEOI amesema hayo leo Jumapili katika duru ya 29 ya Mkutano wa Nyuklia uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti mjini Tehran na kuongeza kuwa, wanasayansi wa nyuklia wa Iran wamepata mafanikio makubwa katika mwaka unaomalizika wa Kiirani wa 1401 Hijria Shamsia, utakaoisha Machi 20.
Amesema Iran imefanikiwa kuzalisha poda maalumu inayotumika kudhibiti kuvuja na kuganda damu wakati wa upasuaji, bidhaa muhimu ambayo Iran ilishindwa kuiagiza kutoka nje ya nchi kutokana na vikwazo vya maajinabi.
Eslami amesema bidhaa hiyo ya tiba inazalishwa hivi sasa kwa wingi na Iran baada ya kupata ridhaa ya Shirika la Chakula na Dawa la Iran, na kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu itaanza kuiuza bidhaa hiyo muhimu nje ya nchi.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imegeukia matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia kwa kutegemea uwezo wa wataalamu wa ndani na imethibitisha kwa nia njema kwamba haina malengo mengine isipokuwa matumizi ya amani na viwanda ya nishati hiyo.
Hivi karibuni, Ali Bahadori Jahromi, Msemaji wa Serikali ya Iran alisema kwamba, Tehran imefanikiwa kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa 500 za tiba kama ambavyo imetoa kibali cha kuzalishwa baadhi ya bidhaa hizo nje ya nchi.