US yaziwekea vikwazo taasisi 39 kwa kuisaidia Iran 'kukwepa' vikwazo vya kifedha
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94934-us_yaziwekea_vikwazo_taasisi_39_kwa_kuisaidia_iran_'kukwepa'_vikwazo_vya_kifedha
Marekani imetangaza kuyawekea vikwazo makumi ya mashirika kwa tuhuma za kuisaidia Iran kukwepa vizingiti vya Washington vya kuiweka Tehran nje ya mfumo wa kimataifa wa fedha.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Mar 10, 2023 04:06 UTC
  • US yaziwekea vikwazo taasisi 39 kwa kuisaidia Iran 'kukwepa' vikwazo vya kifedha

Marekani imetangaza kuyawekea vikwazo makumi ya mashirika kwa tuhuma za kuisaidia Iran kukwepa vizingiti vya Washington vya kuiweka Tehran nje ya mfumo wa kimataifa wa fedha.

Wizara ya Hazina ya Marekani jana Alkhamisi ilitangaza kuziwekea vikwazo taasisi 39 zinazohusika na biashara ya mafuta na bidhaa za petroli za Iran, aghalabu yazo zikiwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu na Hong Kong.

Taarifa ya wizara hiyo ya fedha Marekani imezitaja taasisi hizo kama mtandao wa 'benki kivuli' ambao unayasaidia mashirika ya Iran kuficha biashara zao na wateja wao wa kimataifa, na kufikia mfumo wa kimataifa wa fedha.

Kwa mujibu wa Press TV, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mpaka sasa hawajatoa taarifa wala kuzungumzia vikwazo hivyo vipya vya Marekani.

Haya yanajiri siku chache baada ya Marekani kuyawekea vikwazo makampuni na meli kadhaa katika kuendeleza muelekeo wake wa kiundumakuwili na sera yake ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha wiki iliyopita pia, Marekani iliendelea na uraibu wake huo wa vikwazo kwa kuyawekea vikwazo mashirika 37 ya nchi ambazo hazikubaliani na sera zake za kibeberu. Iliweka vikwazo hivyo kwa kisingizio cha eti kulinda maslahi yake ya kitaifa na kiusalama. 

Wizara ya Fedha ya Marekani iliyawekakwenye orodha yake ya vikwazo  makampuni sita yenye makao yao makuu Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, China na Vietnam pamoja na meli 20 kwa kisingizio cha kuwa na uhusiano na Iran.

Marekani inahesabiwa kuwa nchi inayoongoza kwa uwekaji vikwazo duniani, ikiwa na rekodi kubwa zaidi ya kutumia kila aina ya vikwazo dhidi ya nchi zingine kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yake.