Apr 23, 2023 01:31 UTC
  • Nasser Kanaani Chafi: Ukombozi wa Quds tukufu umekaribia

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ukombozi wa mji mtakatifu wa Quds umekaribia na kwamba, muda si mrefu eneo hilo takatifu litakombolewa na kuondoka katika udhibiti wa utawala ghasibu wa Israel.

Nasser Kanaani Chafi sambamba na kuashiria kwamba, mwaka huu pia Palestina imeng'ara na kutoka kifua mbele iwe ni katika medani ya jihadi au katika uga wa ibada katika msikiti wa al-Aqswa na kueleza kwamba, kila mwaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani malengo matukufu ya Palestina hupata uhai mpya na hivyo kulifanya suala la kukombolewa Quds kukaribia zaidi.

Afisa huyo mwandamizi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mahudhurio ya hamasa ya wananchi wa Palestina katika Sala ya Eidul-Fitr na vilevile ibada mbalimbali katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kubainisha kwamba, ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) zinakabiliwa na machafukko zaidi na wakazi wake wamekata tamaa zaidi kuliko wakati wowote ule.

 

Aidha amesema kuwa, hii leo Wapalestina wana imani zaidi na nusra ya Mwenyezi Mungu na wana uhakika zaidi na matokeo ya muqawama kwa kutegemea himaya na uungaji mkono wa watu huru duniani ambapo dhihirisho la hilo ulikuwa mwangwi uliosikika katika maandamano ya Siku ya kimataifa ya Quds.

Nasser Kanaani ameeleza kuwa, hii leo wanananchi wa Palestina wana matumaini makubwa kuliko wakati mwingine wowote ule ya kuzikomboa ardhi zao na kuitokomeza Israel ambayo ni donda la saratani. 

Tags