Magaidi wakamatwa wakipanga kushambulia maeneo 50 nchini Iran
Waziri wa Usalama Iran Mahmoud Alavi amesema magaidi wakufurishaji waliokamatwa hivi karibuni walipanga kutekeleza mashambulizi katika maeneo 50 kote Iran.
Akizungumza Jumanne, Alavi alisema katika oparesheni kadhaa za usalama mapema katika wiki za hivi karibuni, magaidi 10 Wakufurishaji walikamatwa Tehran na katika mikoa mingine mitatu ya kati mwa Iran.
Ameongeza kuwa, magaidi hao walipanga kuripua mabomu kwa njia ya 'remote control' na pia kutekeza hujuma za kujilipua na kwa mabomu ya kutegwa garini katika maeneo yenye msongamano mkubwa.
Amesema imebainika kuwa magaidi hao walikuwa tayari wameshaainisha maeneo 50 ya kutega mabomu na kwamba tayari walikuwa na kilo 100 za mada za milipuko huku vikosi vya usalama vikifanikiwa kuzuia tani mbili za mada za miripuko ambazo magaidi walipanga kuingiza nchini.
Siku ya Jumatatu Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema vikosi vya usalama nchini vimetibua njama ya kutekelezwa shambulizi la kigaidi hapa mjini Tehran na kuwatia mbaroni watuhumiwa kadhaa wa njama hizo za kigaidi.