Zarif: Mgogoro wa Syria utatuliwe kwa njia ya kisiasa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mgogoro wa Syria unaweza tu kutatuliwa kwa njia ya kisiasa.
Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo huko nchini Ufaransa mbele ya hadhara ya wanadiplomasia wa ngazi ya juu, watafiti na wataalamu wa Kituo cha Kimataifa cha nchi hiyo kuwa, utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria utashindikana iwapo ajenda kuu itahusiana tu na mustakbali wa Rais Bashar Assad wa nchi hiyo.
Zarif amebainisha kuwa mipango ya kisheria ya hapo baadaye inapaswa kupewa uzito atika kadhia ya Syria na kwamba kuasisiwa mfumo wa shirikisho nchini humo halitakuwa suluhisho la mgogoro.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria hali ya mambo katika eneo la Mashariki ya Kati hususan hali ya Yemen, Bahrain, Syria na Iraq na akasema kuhusiana na Bahrain kuwa, moja ya wasiwasi unaolisibu eneo hili ni suala la Bahrain. Amesema hii ni kutokana na kuwa huko Bahrain kundi moja la watu wachache linakandamiza jamii ya walio wengi.