Jun 10, 2023 12:24 UTC
  • Iran yaiasa IAEA isitegemee taarifa za urongo za Israel

Ofisi ya Kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imeutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuwa na msimamo wa kitaalamu kuhusu mradi wa Iran wa nishati ya nyuklia, na kujiepusha na taarifa za urongo za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran mjini Vienna nchini Austria imeeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imejitolea kwa dhati kuendelea kufungamana na Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).

Taarifa hiyo imetolewa baada ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuitumia ripoti Bodi ya Gavana ya wakala huo; ripoti iliyojaa makosa na upotoshaji kwa kutegemea taarifa za urongo za Israel.

Kuhusu kadhia ya kupatikana chembechembe za urani zilizorutubishwa kwa kiwango cha juu, Ofisi ya Kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, Tehran haina mradi wa kurutubisha urani kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 60 na kwamba ni jambo la kawaida kupatikana chembechembe hizo ndogo zilizorutubishwa kwa kiwango cha juu katika maeneo yaliyotajwa na IAEA.

Kadhalika taarifa hiyo imesema kuwa, madai ya Grossi katika ripoti yake kwamba kuna vituo vitatu vya siri ambavyo havijaanishwa hapa nchini kwa ajili ya ukaguzi hayana ukweli wowote, na kwamba Iran imeweka wazi maeneo yake yote, kwa kuwa shughuli yake ya nyuklia ina malengo ya amani.  

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, teknolojia ya nyuklia ni lazima kwa nchi kama Iran yenye idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni 80 kwani teknolojia hii inaweza kukidhi mahitaji yake ya matibabu, na pia kunufaisha viwanda vingine vikubwa vikiwemo vya kuchimba mafuta na kampuni za saruji.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika miaka kadhaa iliyopita umekuwa ukikariri madai yasiyo na msingi yanayotolewa na utawala haramu wa Israel na nchi za Magharibi kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani.  

Hii ni katika hali ambayo, wakaguzi wa wakala huo hadi sasa wametembelea na kukagua mara kadhaa taasisi za nyuklia za Iran lakini hawajawahi kupata ushahidi wala nyaraka zinazothibitisha kuwa miradi ya nyuklia ya Iran inayofanyika kwa malengo ya kiraia imekengekeuka mkondo wa kawaida na inaelekea kuwa ya kijeshi.  

Tags