Magaidi wa ISIS waliibuliwa kuiangamiza Iran lakini kwa nguvu zake imewalemaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i9961-magaidi_wa_isis_waliibuliwa_kuiangamiza_iran_lakini_kwa_nguvu_zake_imewalemaza
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumamosi amesema magaidi wa ISIS waliibuliwa kuiangamiza Iran lakini kwa nguvu zake, Iran imeweza kuwalemaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2016 23:16 UTC
  • Magaidi wa ISIS waliibuliwa kuiangamiza Iran lakini kwa nguvu zake imewalemaza

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumamosi amesema magaidi wa ISIS waliibuliwa kuiangamiza Iran lakini kwa nguvu zake, Iran imeweza kuwalemaza.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo Jumamosi jioni mjini Tehran alipokutana na familia za mashahidi wa tukio la 7 Tir sawa na tarehe 27 Juni na pia familia za mashahidi wa kulinda haram takatifu za Ahul Bayt wa Mtume SAW.

Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu alipongeza Jihadi ya mashahidi na subira ya familia zao na kusema mashahidi ni nguzo ya nguvu za mfumo wa Kiislamu. Amesema njia pekee ya kustawi Iran ya Kiislamu ni kuhuisha moyo wa kimapinduzi na jihadi.

Ayatullah Khamenei mwanzoni mwa kikao hicho ametoa salamu zake za rambi rambi kufuatia kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Ali AS na kusema mtukufu huyo ni shahidi adhimu zaidi katika historia ya mwanadamu na shahidi wa miharabu. Aidha ameashiria tukio la miaka 35 iliyopita wakati bomu lilipolipuliwa katika ofisi ya Chama cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Tehran tarehe 27 Juni mwaka 1981 (7 Tir 1360 Hijria Shamsia) na kusema: "Waliotekeleza jinai hii, baada ya kutoroka Iran, walipewa hifadhi katika nchi za Magharibi zinazodai kupinga ugaidi na kutetea haki za binadamu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kadhia hii ni kashfa kubwa kwa nchi za Ulaya na Marekani. Ameongeza kuwa, kundi la kigaidi lililotekeleza ugaidi huo, MKO, ni la watu waliodai kulinda binadamu na hata kuutetea Uislamu na hivyo kujiunga na mapambano ya taifa la Iran lakini wakafanya kosa kubwa kama hilo la 27 Juni na vitendo vingine vya kigaidi vya kuwaua watu wa kawaida. Amesema kundi hilo hatimaye lilijiunga na mtawala wa kiimla Saddam na sasa linaungwa mkono na Marekani.

Ayatullah Khamenei amesema tukio hilo ni muhimu na lenye funzo lakini la kusikitisha ni kuwa matukio kama hayo hayabainishwi ipasavyo kwa kizazi cha sasa.

Ikumbukwe kuwa Juni 27 mwaka 1981 kufuatia mlipuko katika makao makuu ya Chama cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Tehran, viongozi 72 wa ngazi za juu waliouawa shahidi akiwemo mkuu wa vyombo vya mahakama wakati huo Ayatullah Beheshti.

Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria maudhui ya kulinda haram takatifu za Ahul Bayt wa Mtume SAW huko Iraq na Syria na kusema: "Maudhui hii ni katika maajabu ya historia ambapo vijana wa Iran na nchi zingine ambao wana imani imara wanaacha starehe zao pamoja na wake na watoto wao wadogo na kuenda nchi ya mbali kupigana jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na hatimaye kufikia cheo cha shahada.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuwepo makundi ya magaidi wakufurishaji kama vile ISIS ni kwa ajili ya kukabiliana na mfumo wa Kiislamu. Amesema lengo kuu la kuanzishwa makundi ya magaidi wakufurishaji Iraq na Syria ni kuishambulia Iran lakini kutokana na uwezo na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu, magaidi hao sasa wametumbukia katika kinamasi katika nchi hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria namna utawala wa Bahrain ulivyomlenga Sheikh Isa Qasim na kusema kitendo hicho ni ishara ya ujinga wa utawala wa Manama. Amesema Sheikh Qasim alijitahidi kuzungumza na watu wa Bahrain kadiri alivyoweza na kuwazuia kuchukua silaha lakini utawala wa Bahrain haufahamu kuwa, kumhujumu mwanachuoni huyo mujahidi kuna maana ya kuondoa kizingiti kwa vijana wa Bahrain kuchukua hatua yoyote ile kukabiliana na utawala wa kifalme.