Aug 08, 2023 02:08 UTC
  • Wasiwasi wa Baraza la Usalama kwa hali ya kibinadamu nchini Afghanistan

Akthari ya washiriki katika mkutano wa hivi karibuni wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa chini ya kichwa "Ukosefu wa Usalama wa Chakula Duniani" walionyesha wasiwasi walionao kwa hali ya kibinadamu nchini Afghanistan.

Reena Ghelani, mratibu wa Umoja wa Mataifa katika kitengo cha kupambana na njaa na ukosefu wa usalama katika mkutano huu, alielezea wasiwasi wake juu ya njaa na ukame nchini Afghanistan na kusema kuwa kuendelea kwa migogoro na ukosefu wa usalama bado ni sababu kuu ya njaa na ukame katika nchi hiyo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana, mwaka uliopita raia wa Afghanistan walikuwa katika hali ngumu.

David Miliband, Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji, alisema kuwa, machafuko na ukosefu wa usalama vimekuwa sababu ya kuendelea njaa kwa watu wa Afghanistan. Hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kuzingatia mateso na masaibu ya watu wa Afghanistan inaonyesha kuwa, jumuiya ya kimataifa bado iko makini kwa hali ya kibinadamu ya nchi hii. Pamoja na hayo, hakujachukuliwa hatua za maana na za kimsingi kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi hao na ni kwa sababu hiyo ndio maana hali ya kijamii na kiusalama nchini Afghanistan inaendelea kuzorota siku baada ya siku.

Tukichunguza matamshi ya wawakilishi wa nchi waliohudhuria katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Usalama kilichokuwa na anuani isemayo"Ukosefu wa Usalama wa Chakula Duniani", inaeleweka kabisa kwamba, hakuna suluhisho la kimsingi la kutatua mzozo wa Afghanistan.

Zabihullah Mujahid, mmoja wa viongozi wa serikali ya Taliban

 

Pakistan na India, ambazo ni miongoni mwa nchi zinazoathiri hali ya Afghanistan, hazikupendekeza njia yoyote ya kusaidia kutatua mzozo wa Afghanistan, na baadhi ya nchi pia zilikosoa tu utendaji wa Marekani na washirika wake nchini Afghanistan katika miongo miwili iliyopita.

Arif Akrami, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo: Kutokana na athari za kimataifa kwa matukio ya Afghanistan, nchi hii bado iko kwenye kurunzi ya Baraza la Usalama, lakini kiutendaji na uchukuaji hatua za kivitendo, hakuna uamuzi wowote wa dhati unaochukuliwa kusaidia kutatua mzozo wa nchi hiyo.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, sababu ya hilo ni kuweko tofauti kubwa ya kimtazamo kuhusu matukio ya Afghanistan kati ya wanachama wa Baraza la Usalama.  Wananchi wa Afghanistan wanakabiliwa na hali mbaya katika nyuga mbalimbali hususan dawa, chakula na usalama, matatizo ambayo sehemu yake kubwa inatokana na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na Marekani kwa miongo miwili. Vikwazo vya Marekani, kuporwa takribani dola bilioni kumi katika fedha za Afghanistan na kuzuia Washington kupatiwa Afghanistan misaada ya kiistratejia kutoka kwa mataifa mengine ya dunia ni mambo ambayo yameyafanya matatizo ya nchi hiyo kuwa maradufu.

Wakimbizi wa Afghanistan

 

Ripoti za mashirika ya kimataifa yanayotoa misaada ya kibinadamu kwa Afghanistan, mbali na kutoa indhari kuhusu utapiamlo wa watoto na ukosefu mkubwa wa vyanzo vya kifedha kwa ajili ya kutoa misaada ya kibinadamu, zinaeleza kuwa, hali ya Afghanistan inatia wasiwasi mno.

Muhammad Aamirkhan, mwakilishi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa anasema, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, Waafghani milioni tatu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Hii ina maana kwamba kiwango cha misaada ya kimataifa kwa watu wa Afghanistan kimefikia hatua ya kutisha na wasiwasi kuhusiana na hilo unaongezeka kila siku.

Wengi wanaamini kwamba, uendelezaji wa kilimo mbadala badala ya kasumba, ambao ulipendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zaidi ya miongo miwili iliyopita, bado ni suluhisho bora zaidi la kuiokoa kichakula Afghanistan kutokana na mgogoro mbaya wa sasa inaokabiliwa nao.

Mohsen Rohi-Sefat, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema kuhusiana na suala hilo: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuwa na mtazamo wa kuona mbali kuhusu hali ya Afghanistan, ilipendekeza kilimo mbadala miongo miwili iliyopita na kuchukua hatua, lakini Marekani na Shirika la Kijeshi NATO ambao walikuwa wakiikalia kwa mabavu Afghanistan, hawakuruhusu utekelezaji kamili wa kilimo mbadala, na ni kwa sababu hiyo Afghanistan bado inakabiliwa na shida ya chakula licha ya kuwa na uwezo wa kilimo.

Kwa vyovyote vile, Abdul Latif Nazari, mmoja wa maafisa wa kiuchumi wa serikali ya Taliban, akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama, alitangaza kwamba, kwa maoni ya Taliban, kuibua masuala ya ukosefu wa usalama ni jambo lisilofaa, kwa sababu hapakuwa na vita na mapigano ya kijeshi nchini Afghanistan mwaka uliopita bali ukosefu wa usalama wa chakula ndio ulioshamiri zaidi kutokana na mabadiliko tabianchi, ukame na mafuriko. Hii inaonyesha kwamba Taliban inajaribu kutumia suala la usalama kama mafanikio ya utawala wake na kuikinaisha jamii ya kimataifa kuhusu nguvu ya mamlaka yake hata katika sekta ya kilimo.

Hii ni katika hali ambayo, kundi la Taliban halijafanikiwa kuishawishi jamii ya kimataifa na kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini Afghanistan, na moja ya sababu muhimu za kupungua kwa misaada ya kimataifa kwa Afghanistan ni kukatishwa tamaa na matukio Afghanistan, hususan katika nyanja za kijamii, na kutoshirikiana Taliban na jamii ya kimataifa kuhusiana na hilo.

Hii ni kwa sababu katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili ambayo Taliban imerejea madarakani nchini Afghanistan, sio tu kwamba haijaonyesha harakati na mpango wa maingiliano na jamii ya kimataifa, hasa na majirani wa Afghanistan, bali kwa kuweka vizingiti na mibinyo mikubwa ya kijamii na kielimu, hasa kwa wanawake na wasichana, imeisononesha na kuikatisha tamaa jamii ya kimataifa kuhusiana na mustakabali wa matukio ya Afghanistan.

Tags