Mar 08, 2024 08:30 UTC
  • Hofu ya Wazayuni ya kuibuka Intifadha nyingine Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel una wasi wasi mkubwa wa kuanzishwa Intifadha (mwamko) nyingine ya Palestina katika hali ambayo hauna nguvu na umeonyesha udhaifu mkubwa mkabala wa operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa na makundi ya mapambano ya ukombozi wa Papalestina.

Huku mwezi mtukufu wa Ramadhani ukikaribia, viongozi wa utawala wa Kizayuni wana wasiwasi mkubwa kuhusu kuanzishwa Intifadha kote Palestina, na hasa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza.

Intifadha ni mwamko wa wananchi wa Palestina ulioanza mwaka 1987 ambapo Wapalestina walikabiliana na jeshi la Kizayuni bila ya silaha yoyote. Umuhimu wa Intifadha hiyo ni ushirikiano na umoja mpana kati ya wananchi wa Palestina na makundi ya muqawama yanayosimama pamoja dhidi ya Wazayuni.

Abd al-Bari Atwan, mchambuzi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiarabu, ameashiria matukio ya vita vya Gaza na mafanikio ya makundi ya muqawama, na akasisitiza kwamba: Kadiri tunavyokaribia mwezi wa Ramadhani, ndivyo tunavyozidi kuona nguvu na uimara wa wawakilishi wa muqawama katika mazungumzo ya kusitisha mapigano. 

Mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa pia amesema kwamba mtazamo wa Rais Joe Biden wa Marekani na utawala wa Kizayuni kuhusu uwezo wa makundi ya muqawama wa Palestina si sahihi na ni ghalati.

Abd al-Bari Atwan

Osama Hamdan, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) pia amewataka wananchi wa Palestina kuelekea katika Msikiti wa Al-Aqsa katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem) katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ili wawe sehemu ya mapambano ya Gaza.

Baada ya operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa, kulifanyika vikao vya kwanza vya kubadilishana mateka na usitishaji vita, jambo ambalo liliashiria azma na uwezo wa makundi ya muqawama wa Palestina katika kuendeleza malengo yao na kushindwa kwa utawala wa Kizayuni katika mazungumzo.

Makundi ya wapiganaji wa Kipalestina yanasisitiza matakwa yao ya kutaka utawala wa Israel usitishe kabisa kukaliwa kwa mabavu Gaza na mzingiro wa watu wa eneo hilo.
Lakini kinyume na umoja na mshikamano wa makundi ya muqawama wa Palestina, baraza la mawaziri la  Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel limeshuhudia mgawanyiko na hitilafu kubwa kuhusu kubadilishana mateka na kuendelea vita vya Gaza.
Mashirika ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni pia yamekiri kushindwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita dhidi ya makundi ya muqawama ya Palestina na kubaini kuwa kuendelea vita hivyo kutapelekea Israel ifedheheke zaidi.
Wapalestina, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, katika miaka ya hivi karibuni, daima huanzisha mapambano yao sambamba na kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa namna ambayo utawala wa Kizayuni hushindwa kukabiliana na mapambano hayo.

Osama Hamdan, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas)

Katika miaka ya hivi karibuni, Intifadha imekuwa na nafasi nzuri katika kuvutia hisia za jumuiya ya kimataifa na waungaji mkono wa makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina duniani kote.
Intifadha ya mwaka huu pia inaweza kugeuka kuwa jinamizi kubwa kwa Netanyahu na Wazayuni wenye misimamo mikali.
Utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kukabiliana na kuendelea operesheni za makundi ya muqawama au wapigania ukombozi wa Palestina na umelazimika kurudi nyuma katika maeneo mengi ya vita.
Katika upande mwingine makundi ya muqawama ya Palestina yameweza kutoa vipigo vikubwa kwa Wazayuni kwa kutumia uwezo wao mkubwa wa kiutendaji.

Kuenea mapambano ya wananchi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kunaweza kwa namna fulani kukamilisha mlolongo wa kushindwa mfululizo jeshi la utawala wa Kizayuni. Kwa msingi huo Intifadha ya mwaka huu pia itakuwa sehemu ya kukamilisha mchakato wa "Kimbunga cha Al-Aqsa" iliyoanza tarehe 7 Oktoba, 2023, na Wazayuni kwa kukubali kushindwa, wamekiri kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na makundi ya muqawama ya Palestina.

Tags