Mar 08, 2024 11:15 UTC
  • Wazayuni waendeleza jinai za mauaji na uteketezaji wa miundombinu katika maeneo tofauti ya Ghaza

Kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza kumepelekea kuongezeka idadi ya Wapalestina wanaouawa shahidi na miundombinu inayobomolewa na kuteketezwa katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Shahab, Wizara ya Afya ya Ghaza imetangaza katika taarifa kwamba katika muda wa saa 24 zilizopita, utawala wa Kizayuni umefanya jinai tisa mpya katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza, ikiwemo Khan Yunis na Rafah, kwa kuua watu 83 na kujeruhi wengine 142.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, utawala wa Kizayuni umeshambulia pia kwa mabomu na makombora maeneo mbalimbali ya Jabalia na Beit Lahia na eneo la Al-Salatin kaskazini mwa Ghaza na kuua shahidi Wapalestina kadhaa.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya Ghaza imesema: wakijumuishwa Mashahidi wapya, idadi ya Wapalestina waliouliwa shahidi kutokana na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel tangu utawala huo haramu ulipovamia Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023, hadi sasa imefikia karibu watu 31,000.

Wakati huohuo Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetoa taarifa ikitangaza kuuawa shahidi wafungwa 27 wa Kipalestina katika jela za utawala wa Kizayuni kutokana na mateso makali.

Taarifa hiyo imetilia mkazo ulazima wa Jamii ya Kimataifa kuingilia kati kwa ajili ya kulihami mkono taifa la Palestina dhidi ya jinai zinazofanywa kwa malengo maalumu na utawala wa Kizayuni hususan katika Ukanda wa Ghaza na kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya kusimamishwa hujuma za kijeshi za utawala wa Kizayuni katika Ukanda huo na kuzuia mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo.

Wakati huo huo, Sigrid Kag, mratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa huko Ghaza, amesisitiza mwishoni mwa mkutano wa Baraza la Usalama la umoja huo kuhusu umuhimu wa vivuko vya nchi kavu kwa ajili ya kufikisha misaada kwa watu akisema, kutuma misaada ya kibinadamu huko Ghaza kwa njia ya angani au baharini hakuwezi kuwa chaguo mbadala la vivuko vya ardhini, hasa kwa vile misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ghaza inahitaji kuendelea kupelekwa kwa kipindi kirefu katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, baada ya kupita zaidi ya miezi mitano ya vita na mzingiro mkali iliowekewa Ghaza, wakazi wengi wa eneo hilo wanakabiliwa na baa la njaa kali.../

 

Tags