Mar 21, 2024 14:07 UTC
  • Palestina: Safari za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika eneo hazina tija yoyote

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema diplomasia inayofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani Anthony Blinken katika Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) bado haijatoa "matokeo yoyote ya kuonekana" kwa ajili ya Ghaza.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema, badala yake, diplomasia hiyo ya Blinken inaupa utawala wa Kizayuni wa Israel muda zaidi wa kushadidisha uvamizi na jinai zake dhidi ya Wapalestina.
 
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imebainisha katika taarifa yake kwamba, "Serikali ya Israel inaitumia fursa ya kutopatikina mafanikio, uwezo wake wa kuzungumza na kutoa taarifa ili kupata muda zaidi wa kukamilisha mafanikio ya malengo yake makuu ya uvamizi dhidi ya watu wa Palestina".
 
Blinken, ambaye kwa sasa yuko katika safari yake ya sita ya Asia Magharibi tangu vilipoanza vita vya kikatili vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza, alisema jana kuwa utawala huo na harakati ya Hamas zinapiga hatua kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano.

Baada ya kuzuru Saudi Arabia hapo jana, waziri wa mambo ya nje wa Marekani ameelekea Misri leo kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zingine za Kiarabu na afisa mwandamizi wa Palestina.

 
Akiwa nchini Saudia, Blinken alitangaza kuwa Marekani imesambaza rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka "kusitishwa mara moja kwa mapigano ili kufanikisha kuachiliwa kwa mateka".
 
Ameongeza kuwa, Washington ina matumaini makubwa ya azimio hilo kuungwa mkono na nchi wanachama.
 
Marekani, ambayo ndiye mfadhili na muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, huko nyuma ilishatumia mara kadhaa kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia chombo hicho kikuu cha kimataifa kisipitishe azimio la kusitishwa mara moja mapigano katika ardhi ya Palestina.
 
Tangu walipokwamisha rasimu ya azimio lililopendekezwa na Algeria la kutaka "kusitishwa mara moja mapigano kwa sababu za kibinadamu" huko Ghaza mwishoni mwa mwezi wa Februari, maafisa wa Marekani wamekuwa wakijadiliana kuhusu rasimu mbadala inayolenga kuunga mkono juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki sita ili kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni.../

Tags