Mar 26, 2024 12:32 UTC
  • Kuendelea jinai za Israel: Unyakuzi mkubwa zaidi wa ardhi za Ukingo wa Magharibi tangu 1993

Licha ya kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa mpango wa Israel wa kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria, lakini katika hatua mpya, utawala unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu umenyakua ardhi ya hekta 800 katika Bonde la Jordan kwenye Ukingo wa Magharibi kwa ajili ya ujenzi wa mamia ya nyumba za walowezi.

Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa Israel, ambaye ametia saini azimio la kunyakua ardhi hizo, amesema: Tangazo la kutwaliwa ardhi hiyo ni suala muhimu na la kimkakati, na imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mamia ya nyumba za makazi, viwanda na maeneo ya biashara na ajira.

Hatua hiyo ya Israel imekuja katika hali ambayo Umoja wa Mataifa na nchi nyingi za dunia zinatambua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kuwa ni kinyume cha sheria. Kwa sababu utawala ghasibu wa Israel ulivamia na kuzikaliwa kwa mabavu ardhi hizi katika vita vya 1967, na kwa kuzingatia Mkataba wa Geneva, ni marufuku kufanya ujenzi wa aina yoyote katika ardhi zinazovamiwa na kukaliwa kwa mabavu. Hata hivyo mamia ya maelfu ya Wazayuni hivi sasa wanaishi katika vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi vilivyojengwa na utawala wa Kizayuni baada ya vita vya mwaka 1967 na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Mashariki mwa Quds (Jerusalem).

Sasa, katika hatua nyingine, Israel inajaribu kupora sehemu nyingine ya ardhi ya Palestina. Kundi lenye siasa kali za mrengo wa kulia katika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu limekuwa likitekeleza rasmi sera ya kutwaa ardhi za Palestina katika Ukingo wa Magharibi tangu mwaka 2023; na vita vya Gaza na hali ya sasa ya Wapalestina vimetoa fursa zaidi kwa wavamizi kunyakua ardhi zaidi. Kitendo hiki kimepingwa hata na washirika wa Israel.

Utawala haramu wa Israel unaendelea kunyakua ardhi ya Palestina

Umoja wa Ulaya umelaani vikali uamuzi wa Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, wa kunyakua ardhi zaidi ya Palestina yenye ukubwa wa hekta 800. Peter Stano, msemaji wa sera ya mambo ya nje ya Umoja wa Ulaya pia ametangaza katika taarifa yake kwamba: Huu ni unyakuzi mkubwa zaidi wa ardhi ya Palestina tangu kusainiwa makubaliano ya Oslo kati ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na utawala ghasibu wa Israel mnamo 1993. Stano amesisitiza kuwa: Kupanuliwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina ni ukiukaji wa wazi na wa hatari wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Ijapokuwa viongozii wengine wa nchi za Ulaya akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani wamelaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kujenga vitongoji vipya vya walowezi katika maeneo tofauti ya Palestina, lakini hawajachukua hatua yoyote ya dhati kukomesha jinai hiyo inayofanywa na Israel. Katika muktadha huu, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amelaani mpango huo mpya wa Israel na kutangaza kuwa: Kuwalazimisha Wapalestina kuondoka Rafah ni uhalifu wa kivita. Macron amesema ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina ni ukiukaji wa wazi na hatari wa sheria za kimataifa.

Kwa upande wake, Volker Türk, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa: Kujenga na kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni jinai na uhalifu wa kivita na kunaweza kuharibu uwezekano wowote wa kuanzisha taifa imara la Palestina.

Licha ya maonyo na msimamo huo wa kimataifa wa kulaani sera ya Israel ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizonyakuliwa za Palestina, Israel ingali inasisitiza juu ya kuendelezwa sera hiyo, na inaonekana kuwa ni moja ya stratijia muhimu za utawala huo ghasibu baada ya kufeli sera zake dhidi ya Wapalestina.

Israel inaendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi

Netanyahu na baraza lake la mawaziri ambao wako chini ya mashinikizo makubwa ya ndani hawajaweza kupata mafanikio ya maana ikiwa ni pamoja na kukomboa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na makundi ya ukombozi ya Palestina licha ya kupita miezi sita sasa tangu kuanza vita vya Gaza. Hivyo wameamua kutekeleza sera ya kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina huko Ukingo wa Magharibi ili asaa wakafidia kushindwa kufikia malengo yao yalioainishwa hapo awali kuhusiana na vita vya Gaza.