Ijumaa 15 Julai 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 10 Shawwal 1437 Hijria inayosadifiana na 15 Julai 2016.
Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 15 Julai 1944, ndege za kivita za jeshi la anga la Marekani zilianzisha mashambulizi makubwa huko Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Ndege za kivita za Marekani aina ya B-29 zilishiriki kwenye mashambulizi hayo kwa kurusha makombora katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Mashambulizi hayo yaliharibu viwanda zaidi ya elfu tatu vya Japan vikubwa kwa vidogo na kuuwa kwa umati makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo.
Tarehe 15 Julai miaka 112 iliyopita alifariki dunia Anton Chekhov aliyekuwa mwandishi mashuhuri wa riwaya na michezo ya kuigiza wa karne ya 19 nchini Russia. Chekhov pia alikuwa tatibu na alianzia zahanati ya kutoa matibabu ya bure kwa watu wasiojiweza ambako alitoa huduma hiyo yeye mwenyewe. Umahiri wa Anton Chekhov ulikuwa katika kuandika riwaya na visa vifupi. Falsafa yake ilijengeka juu ya msingi wa kuishi maisha ya chini na ya watu wa kawaida na daima alikuwa akisema: Kuhisi furaha na saada ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu. Aliamini kuwa iwapo mwanadamu ataongozwa vizuri katika kipindi cha ujana hapana shaka atakuwa na maisha mazuri na yasiyo na taabu. Ivanov", "The Seagull", "Uncle Vanya", "Three Sisters" na "The Cherry Orchard" ni miongoni mwa vitabu vya visa na michezo ya kuigiza vya mwandishi huyo mashuhuri.
Na siku kama ya leo miaka 428 kulitokea vita vya Bahari ya Manche (English Channel) kati ya jeshi la majini la Uhispania maarufu kama Jeshi la majini lisiloshindwa na jeshi la majini la Uingereza. Katika vita hivyo meli kubwa 135 za kivita za Uhispania ziliishambulia Uingereza kwa shabaha ya kulipiza kisasi cha mauaji ya malkia Mary Stuart wa Scotland lakini kutokana na kimbunga kikali meli 85 za Uhispani zilizama majini na kikosi cha jeshi la majini kisichoshindwa cha Uhispania kikapata kipigo kikubwa. Tangu wakati huo nyota ya na umashuhuri wa kikosi hicho ikaanza kuzama.