Jan 12, 2017 09:09 UTC
  • Rafsanjani, Mwanasiasa wa Aina Yake-1

Habari iliyotangazwa saa moja na nusu usiku wa Jumapili tarehe 8 mwezi huu wa Januari kwa wakati wa Tehran iliwatia simanzi na huzuni kubwa mamilioni ya Wairani na wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika pembe mbalimbali za dunia.

Ayatullah Hashemi Rafsanjani

Usiku huo ilitangazwa habari ya kufariki dunia aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani ambaye alikuwa mmoja kati ya vinara wa mapambano dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah na miongoni mwa wasaidizi wa Imam Ruhullah Khomeini. Katika ujumbe wake wa taazia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema: Ni suala gumu na lenye kuumiza mno kumpoteza mwanamapambano mwenzangu na mshirika ambaye ushirikiano wetu una umri wa miaka 59. Tumekumbana na mashaka na misukosuko mingi sana katika makumi hayo ya miaka na kushirikiana katika fikra katika vipindi vingi na kustahamili hatari nyingi katika njia ya pamoja. Uhodari wake mkubwa na upendo nadra kuonekana katika miaka hiyo ulikuwa egemeo la kutegemewa kwa wale wote walioshirikiana naye hususan mimi.." Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusifia shakhsia ya Ayatullah Rafsanjani kwa kusema: Alikuwa mtu mwenye mifano michache kati ya kizazi cha awali cha wanamapambano dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah na miongoni mwa waliopata mashaka makubwa katika njia hiyo yenye hatari na fahari kubwa. Miaka mingi ya kufungwa jela na kustahamili mateso ya Savak (shirika la usalama la utawala wa Shah) na kusimama kwake kidete mkabala wa hayo yote, majukumu mazito katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, uspika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na uongozi wa Baraza la Watalaamu na kadhalika, yote ni kurasa zinazong'aa za kitabu cha maisha yaliyojaa misukusuko ya mwanamapambano huyu mkongwe", mwisho wa kunukuu.    

Ali Akbar Hashemi Rafsanjani alizaliwa mwaka 1935 katika kijiji cha Bahreman katika wilaya ya Rafsanjan kwenye mkoa wa Kerman. Alizaliwa kwenye familia ya wakulima na yenye asili na historia ya kidini. Aliekelea katika mji mtakatifu wa Qum akiwa na umri wa miaka 14 kwa ajili ya kupata elimu ya dini. Kijana Ali Akbar aliyekuwa na shauku kubwa ya kupata elimu na maarifa ya Kiislamu, aliingia mapema katika medani ya mapambano ya kisiasa. Ali Akbar Hashemi Rafsanjani   alianza harakati zake za kisiasa na kiutamaduni baada ya mapinduzi ya Marekani na Uingereza dhidi ya serikali ya Dakta Musaddiq hapa nchini hapo mwaka 1953. Kipindi hicho ndipo alipokutana na kujuana na Ayatullah Ali Khamenei. Hata hivyo kitu kilichofungua ukurasa mpya katika maisha ya kijana Ali Akbar ni kufahamiana kwake na Imam Ruhullah Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu. Wakati huo Imam Khomeini alikuwa bado hajajulikana kama marjaa na kiongozi wa kidini anayefuatwa katika masuala ya kisheria na fatwa na hakuwa mashuhuri sana miongoni mwa wananchi wa Iran. Hata hivyo alihesabiwa kuwa miongoni mwa wahadhiri na walimu hodari katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum. Taratibu, Ali Akbar Rafsanjani alianza kuingia katika vikao vya kundi la wanafunzi wa karibu kwa Imam Ruhullah Khomeini. Sambamba na kutafuta elimu na kuendeleza mapambano, Akbar Hashemi Rafsanjani hakuacha kazi za kulingania elimu, maarifa na mafundisho ya Uislamu na alianza kutoa jarida la Madhehebu ya Shia akishirikiana na vijana kadhaa waliokuwa wakitafuta elimu na maarifa katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum.

Baada ya mapinduzi ya serikali ya Dakta Musaddiq hapo mwaka 1953 yaliyosimamiwa na Marekani na Uingereza, mfalme Muhammad Reza Pahlavi alifanya jitihada kubwa za kuimarisha misingi ya utawala wake, na kutokana na kwamba hakuwa akiungwa mkono na sehemu kubwa ya wananchi, Shah alifanya kila awezalo kuwa tegemezi zaidi kwa mkoloni mkongwe yaani Uingereza na vilevile Marekani. Katika mkondo huo alichukua hatua za kufanya mabadiliko katika sheria za nchi na kufanya marekebisho ya ardhi chini ya mwavuli wa kile alichokiita "Mapinduzi Meupe" na kuelekea kwenye milango ya ustaarabu mkubwa. Hata hivyo marekebisho hayo kwa hakika yalifanyika kwa ajili ya kuvuruga utamaduni na dini ya watu wa Iran na kutayarisha uwanja mkubwa zaidi wa istiimari na unyonyaji wa nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza nchini Iran.

Maandamano ya wananchi wa Iran dhidi ya Shah

Baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi aliyekuwa kiongozi mkuu wa kidini katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum, Imam Khomeini alianza kutajwa kama mmoja kati ya wanazuoni marejeo na wakuu wa kidini nchini Iran na wananchi wengi wakaanza kurejea kwake katika masuala ya sheria na fiqhi. Imam Ruhullah Khomeini aliyekuwa amezungukwa na wanafunzi shujaa na wanamapambano kama Hashemi Rafsanjani, aliendelea kuwazindua wananchi wa Iran kuhusu malengo ya utawala wa Shah kwa ajili ya kuimarisha ukoloni na unyonyaji uliokuwa ukifanyika kwa anwani ya marekebisho ya ardhi na Mapinduzi Meupe. Hotuba za Imam Khomeini katika kipindi hicho ambazo zilifichua uovu na dhulma za utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi, zilitikisa misingi ya utawala huo. Shah alizidisha mbinyo, mateso na kuwatia nguvuni wanaharakati wa kisiasa na kidini na kutengeneza anga ya ukandamizaji kwa ajili ya kuzima harakati za Imam na wafuasi wake.

Mwaka 1963 utawala wa Shah awali ulivamia na kushambulia shule kubwa na maarufu zaidi ya kidini ya Faidhia katika mji wa Qum na kuua na kujeruhi mamia watu. Vilevile uliwatia nguvuni wanafunzi wengi akiwemo Akbar Hashemi Rafsanjani. 

Shule ya kidini ya Faidhiya, Qum

Kipindi hicho wanafunzi wa vyuo vya kidini waliondolewa jukumu la kutoa huduma jeshini. Hata utawala wa Shah aliamua kuwalazimisha wanafunzi wa vyuo vya kidini kwenda kutoa huduma jeshini kwa shabaha ya kuwaweka mbali na vyuo vya kidini vilivyokuwa vituo vikuu vya harakati za mapambano chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini. Hashemi Rafsanjani alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza wa kidini waliopelekwa kutoa huduma jeshini.  

Mapambano ya moja kwa moja ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah yalianza baada ya tukio la tarehe 15 Khordad. Mamia ya watu waliuawa, wengine kujeruhiwa na baadhi yao walitiwa nguvuni na vyombo vya jeshi na usalama vya Shah. Baada ya tukio hilo, Hashemi Rafsanjani ambaye alikuwa amepewa ruhusa ya kutembelea familia yake hakurudi tena kambini na aliishi maisha ya kujificha kwa miezi kadhaa katika eneo alikozaliwa la Rafsanjan. Katika kipindi hicho ndipo alipofasiri na kutarjumu kitabu cha Historia ya Palestina kilichoandikwa na Akram Zuaiter.

Kitabu cha Historia ya Palestina

Tarjumi ya kitabu hicho ilichapishwa ikiwa na utangulizi ulioandikwa na Hashemi Rafsanjani ambao kwa hakika ulikuwa sauti ya malalamiko dhidi ya ubeberu wa ndani ya Iran na ukoloni wa kigeni na dhihirisho la hali ya Waislamu hususan watu wanaodhulumiwa wa Palestina. Tarjumi hiyo ya kitabu cha Historia ya Palestina ilikuwa na taathira kubwa katika tabaka la wasomi na wanamapambano katika siku hizo.

Mapambano ya Hashemi Rafsanjani na wanafunzi wengine wa Imam Khomeini yaliingia katika awamu mpya baada ya Ayatullah Ruhullah Khomeini kupelekwa uhamishoni nchini Uturuki na baadaye Iraq, Novemba mwaka 1964.

Imam Khomeini akiwa uhamishoni nchini Uturuki

Ali Akbar Hashemi Rafsanjani kama walivyokuwa wanafunzi wengine wa Imam Ruhullah na wanaharakati wa kisaisa na kidini dhidi ya utawala wa Shah, walikuwa wakifuatiliwa na utawala wa Shah. Alikamatwa mara kadhaa na kuteswa vikali na shirika la usalama la Shah maarufu kwa jina la Savak ambalo lilikuwa miongoni mwa mashirika ya usalama na ujasusi ya kutisha zaidi ya katika kipindi hicho. Hata hivyo mateso na ukandamizaji huo haukuwa na taathira katika azma na irada imara ya Rafsanjani na wanafunzi wengine wa Imam Khomeini katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kifalme wa Iran. Ali Akbar Hashemi Rafsanjani hakulegalega hata kidogo au kuonesha udhaifu hata alipokuwa katika mateso ya Savak katika jela za utawala wa Shah. Alitumia wakati huo wa kushikiliwa korokoroni kuandika vitabu na makala zilizolingania maarifa ya Kiislamu baina ya wafungwa wenzake.  

Wakati alipokuwa nje ya jela pia Hashemi Rafsanjani aliendeleza harakati zake za kisiasa na kidini dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah na alilitambua suala la kuzisaidia kifedha familia za wafungwa kuwa ni jukumu na wajibu wake. Alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa harakati za mapambano. Vilevile alikuwa na uhusiano na mawasiliano ya karibu sana na Imam Ruhullah Khomeini  huko Iraq na baadaye Paris wakati wa kilele cha maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah. Jina la Rafsanjani pia lilionekana mwanzoni mwa orodha ya majina yaliyopasishwa na Imam Khomeini kwa ajili ya kuainisha wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Ransanjani akiwa pamoja na Imam Ruhullah Khomeini

Kama ambavyo Hashemi Rafsanjani alivyokuwa mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya utawala wa Shah na kati ya wanafunzi wa karibu wa Imam, vilevile alikuwa nafasi muhimu katika kuimarisha nguzo na misingi ya Mapinduzi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika kipindi chetu kijacho kutatupia jicho mchango wa Ayatullah Hasheni Rafsanjani katika harakati za maendeleo ya Iran na maisha yake ya kisiasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.        

   

Tags