Matakwa mapya ya kufanyiwa marekebisho muundo wa Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i34581-matakwa_mapya_ya_kufanyiwa_marekebisho_muundo_wa_umoja_wa_mataifa
Ikiwa ni katika harakati mpya, wawakilishi wa nchi 128 wametia saini mpango wa kutaka marekebisho yafanyike katika muundo wa Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 19, 2017 23:21 UTC

Ikiwa ni katika harakati mpya, wawakilishi wa nchi 128 wametia saini mpango wa kutaka marekebisho yafanyike katika muundo wa Umoja wa Mataifa.

Katika tukio jingine pia, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutaja "urasimu" kuwa ndio tatizo kubwa la umoja huo na akatangaza himaya yake kwa suala la kufanyiwa marekebisho muundo wa jumuiya hiyo kubwa zaidi ulimwenguni. Kimsingi ni kuwa, mabadiliko katika muundo wa Umoja wa Mataifa inahesabiwa kuwa daghadagha na sumbuko kubwa zaidi la taasisi hiyo ya kimataifa.

Hapana shaka kuwa, kufanyiwa mabadiliko muundo wa sasa wa Umoja wa Mataifa ambao ni urithi uliobakia wa kipindi cha vita baridi ambao hautabikiani wala kuoana na uhakika na muundo wa sasa wa ulimwengu ni jambo lenye umuhimu mkubwa zaidi hii leo ambapo walimwengu wanashuhudia mabadiliko ya mifumo ya kimataifa kuelekea upande wa kambi kadhaa.

Nembo ya Umoja wa Mataifa

Katika miaka ya nyuma kulifanyika juhudi kubwa na za kila upande kwa ajili ya kuhakikisha kunakuweko mabadiliko katika muundo wa Umoja wa Mataifa na hivyo kuboresha nafasi ya umoja huo katika kutatua matatizo na migogoro ya kimataifa.

Hata hivyo ubunifu wa kutaka kuweko mabadiko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama vile kuongezwa idadi ya wanachama wa kudumu katika baraza hilo au kufutwa kura ya veto, hadi sasa ni mambo ambayo bado hayajakubaliwa na kuafikiwa na nchi zote. 

Ni kwa mintarafu hiyo ndio maana nchi nyingi hususan zilizoendelea kiviwanda duniani kama Ujerumani, Japan na nchi zinazochomoza kiuchumi kama Brazil, India na Afrika Kusini zikataka kutazamwa upya muundo wa taasisi hiyo na kuweko muundo mpya ambao utaendana na uhakika wa sasa ulimwenguni. Said Mahmoudi mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uga wa sheria za kimataifa anasema kuwa:

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Katika miongo miwili iliyopita nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika juhudi za kidiplomasia za kutaka kuweko mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa kiidara na utendaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni Brazil, Ujerumani, Japan na India. Hata hivyo juhudi hizo hadi sasa hazijazaa matunda kutokana na upinzani wa madola yenye nguvu na yenye ushawishi ndani ya umoja huo.

Ukweli wa mambo ni kuwa, utambulisho wa ukosoaji kuhusiana na muundo na utendaji wa Umoja wa Mataifa unatofautiana kikamilifu miongoni mwa nchi wanachama wa umoja huo.

Marekani inataka kuweko Umoja wa Mataifa kwa sura ambayo itaweza kusukuma mbele gurudumu la matakwa yake na ndio maana siku zote haiwezi kuvumilia hatua na misimamo huru kama ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM.

Russia ni miongoni mwa nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Lakini kwa upande wa wanachama wa kawaida wa Umoja wa Mataifa hususan zile nchi ambazo zinataka kuwa na nafasi muhimu zaidi katika Baraza la Usalama, zinakosoa kupewa haki ya veto nchi tano tu wanachama wa kudumu wa baraza hilo na ndio maana zimekuwa zikitaka kufafanuliwa tena maana na fasili ya muundo wa taasisi hiyo hasa Baraza la Usalama likiwa ndiyo nguzo ya kiutendaji na kiusalama ya taasisi hiyo.

Kazem Gharibabadi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuwa: Haki ya veto ni miongoni mwa mambo ambayo daima yamekuwa changangoto na chimbuko kubwa la malalamiko miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Ukweli ni kuwa, muundo wa sasa wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukiandamwa na wimbi la ukosoaji wa nchi nyingi na mpangilio wa sasa hususan wa wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hautakiwi na nchi nyingi duniani.

Marekani, Russia, China, Ufaransa na Uingereza ni nchi tano zenye haki ya kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Kwa kuzingatia muundo wa hivi sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baadhi ya mabara na maeneo ya dunia hayana mwanachama na mwakiilishi wa kudumu katika baraza hilo.

Miongoni mwa mabadiliko ambayo yamekuwa yakitakiwa mno na nchi mbalimbali katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kufanyiwa marekebisho muongozo wa utendaji, kufutwa kura ya veto na kuongezwa idadi ya wanachama wa kudumu katika baraza hilo.

Tukirejea nyuma tunaona kuwa, Baraza la Usalama ambalo liliundwa miaka 72 iliyopita kwa lengo la kile kilichoelezwa kuwa kwa ajili ya kutetea usalama wa dunia, hadi leo licha ya kupita miaka yote hii na pamoja na kutokea mabadiliko mengi ya kimsingi duniani katika kipindi chote hiki, lakini muundo wa taasisi hiyo haujabadilishwa hadi leo, bali umebakia kuwa vile vile.