Ombi la Umoja wa Mataifa la kuanza mazungumzo nchini Togo
Kufuatia kushtadi na kupanuka mgogoro wa kisiasa wa Togo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka serikali na makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo kufanya mazungumzo chanya yatakayolikwamua taifa hilo kwenye mgogoro huo wa kisiasa.
Antonio Guterres alitoa ombi hilo alipokutana hivi karibuni na Komi Selom Klassou, Waziri Mkuu wa Togo ambapo aliitaka serikali na wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo kufanya marekebisho ya msingi ya kisiasa nchini humo. Ni kwa muda sasa ambapo Togo imekuwa uwanja wa malalamiko ya vyama vya upinzani. Familia ya Gnassingbé imekuwa ikiiongoza nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kwa miongo mitano mfululizo. Rais wa sasa Faure Gnassingbé naye amekuwa madarakani tangu alipofariki dunia baba yake, Gnassingbé Eyadém mwaka 2005 ambaye naye aliitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 38 hadi alipofariki dunia. Kwa sasa pendezo la serikali la kuifanyia marekebisho katiba na kadhalika kutekelezwa baadhi ya marekebisho ya kisiasa nchini humo, limeibua hasira kali ya wapinzani.
Wapinzani wanaamini kwamba chama tawala kinakusudia kufanya marekebisho ambayo yatambakisha madarakani Rais Faure Gnassingbé. Suala hilo ndilo limesababisha maandamano na mikusanyika ya kila mara ya malalamiko kutoka kwa wapinzani sambamba na makabiliano kati ya jeshi la polisi na waandamanaji. Katika hali hiyo, Denis Amouzou Dzakpa Askofu Mkuu wa kanisa kuu la Lomé, mji mkuu wa Togo sambamba na kuonyesha masikitiko yake kutokana na kushtadi migogoro ya kisiasa katika wiki za hivi karibuni na kadhalika kuendelea ukandamizaji wa maafisa usalama dhidi ya waandamanaji, ametaka kutatuliwa mzozo huo wa ndani kwa kufanyika marekebisho na kutekelezwa upya katiba ya mwaka 1992. Wapinzani wa serikali wanataka kutekelezwa upya katiba iliyopitishwa mwaka 1992 ambayo inaainisha kipindi anachoweza kuongoza rais. Kwa mujibu wa wapinzani, Rais Faure hana haki tena ya kugombea katika uchaguzi ujao nchini humo.
Katika mabadiliko ya sasa, hata kama pendekezo la ukomo wa rais limejumuishwa, lakini chama tawala kinaamini kuwa, ikiwa marekebisho hayo yatapitishwa, basi rais wa sasa atakuwa na haki ya kugombea tena katika uchaguzi ujao. Pendekezo la marekebisho ya katiba ya Togo lilikuwa limepangwa kupigiwa kura ya maoni na wananchi hivi karibuni. Juhudi za kuendelea kusalia madarakani kwa kipindi kirefu, zimekuwa zikifanywa na viongozi wa nchi nyingi za Kiafrika. Udhaifu wa kiutamaduni na kisiasa, kukosekana uthabiti wa kisiasa na kidemokrasia, kutokita mizizi ya kidemokrasia katika jamii, nafasi ya ukabila na kadhalika uungaji mkono wa nyuma ya pazia wa baadhi ya nchi za Magharibi kwa watawala walioko madarakani, ni kati ya mambo yanayowasukuma baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika kuendelea kung'ang'ania madaraka. Katika njia hiyo akthari ya viongozi hao hutumia mabadiliko ya katiba, kuondoa ukomo wa vipindi vya uongozi au kuamua kubakia tu madarakani kupitia njia za hadaa za mazungumzo, kama ilivyojiri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hii ni katika hali ambayo kupitia uhamasishaji wa vyama vya kisiasa na kuongezeka kiwango cha uelewa wa raia wa nchi tofauti za Kiafrika, wananchi hao wamekuwa wakipinga mwenendo huo wa watawala na wanataka kuimarishwa demokrasia ili kufikia haki zao za kimsingi. Kuhusiana na suala hilo, Hervé Bourges mtaalamu wa masuala ya Afrika anasema: "Licha ya kwamba demokrasia ni sharti la kwanza, lakini bado akthari ya nchi za bara la Afrika zinaendelea kutawaliwa kidikteta na kwa msingi huo, haziwezi kustawi madamu demokrasia haipewi nafasi ya kuenea." Mwisho wa kunukuu. Katika mazingira hayo inasubiriwa kuona iwapo mwito wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kufanyika mazungumzo yenye lengo la kuhitimisha tofauti za kisiasa nchini Togo, utaitikiwa au la.