Haja ya Taliban kutafakari upya vizuizi vya maombolezo ya Muharram
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100274-haja_ya_taliban_kutafakari_upya_vizuizi_vya_maombolezo_ya_muharram
Baraza la Maulamaa wa Kishia wa Afghanistan limeitaka serikali ya wanamgambo wa Taliban kufikiria upya baadhi ya mibinyo na vikwazo ilivyoweka vya kufanya maombolezo ya Muharram.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2023 11:01 UTC
  • Haja ya Taliban kutafakari upya vizuizi vya maombolezo ya Muharram

Baraza la Maulamaa wa Kishia wa Afghanistan limeitaka serikali ya wanamgambo wa Taliban kufikiria upya baadhi ya mibinyo na vikwazo ilivyoweka vya kufanya maombolezo ya Muharram.

Baraza hilo limetangaza katika taarifa yake kwamba, maafisa wa serikali ya Taliban walizungumzia suala la kuzuia na kuweka sheria na mibinyo katika maeneo na katika ratiba za maombolezo ya Muharram kutokana na vitisho vya usalama katika kikao na wajumbe wa kamati ya usimamizi ya Muharram. Lakini katika kikao kilichohudhuriwa na mkuu na wajumbe wa Baraza la Maulamaa wa Kishia pamoja na wanazuoni watajika wa Kishia, pendekezo la maafisa wa serikali la kutekeleza vizuizi vya kufanya maombolezo ya Muharram lilikataliwa na kukateuliwa ujumbe wa watu saba kwa ajili ya kwenda kufanya mashauriano maafisa wa serikalii ya Taliban na kuwafikishia ujumbe wa Mashia wa Afghanistan.

Vizuizi hivyo vinawekwa katika hali ambayo, viongozi wa kisiasa, kijeshi na kieneo wa serikali ya Taliban wamesisitiza mara chungu nzima kwamba, wanaheshimu na kuchunga haki za Waislamu wa Kishia hususan uhuru wa kufanya marasimu na maombolezo ya kukumbuka kifo cha Imamu Hussein bin Ali (as) katika mwezi wa Muharram.

Kwa muktadha huo, uamuzi wa Taliban wa kuweka vizuizi na mibinyo katikka maombolezo ya Muharram unaweza kuwa na sababu kadhaa:

 

Sababu ya Kwanza; uamuzi huu unaonyesha kutokuweko msimamo mmoja baina ya wajumbe wa serikali ya Taliban katika uchukuaji maamuzi.

Sababu ya Pili; serikali ya Taliban kinyume na madai yake haina itikadi ya kweli na suala la kuheshimu haki za Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Sababu ya Tatu; kutokuwa na uwezo wa kudhamini usalama katika hafla na maombolezo ya Waislamu wa Kishia katika mwezi huu wa Muharram.

Na sababu ya nne ni kwamba, wanamgambo wa Taliban wanakusudia kudhoofisha itikadi hii ya kimadhehebu nchini Afghanistan na badala yake kuweka itikadi zao.

Arif Akrami, mweledi na mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na kadhia hiii kwamba:

Kila mwaka, maombolezo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imamu Hussein (as) hufanyika kwa mahudhurio makubwa ya watu wa Afghanistan, na watu kutokana na huba na mapenzi waliyonayo kwa Bwana huyu wa mashahidi, husaidia kudhamini usalama wa maombolezo hayo. Minratafu hiyo, licha ya kuwa kudhamiini suala la usalama kwa ajili ya maombolezo ya Muharram ni muhimu, lakini haionekani kama Taliban hawana uwezo kudhamini hilo.

Ni kwa sababu hiyo, ndio maana Baraza Maulamaa wa Kishia wa Afghanistan sanjari na kuthamani ushirikiano wa hapo kabla wa Taliban, limeitaka serikali ya wanamgambo hao kutafakari upya vizuizi tajwa ili waombolezaji wa Imamu Husseini (as) waweze kufanya maombolezo hayo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kwa kuzingatia kwamba Imamu Husein (as.) na Ahlul-Bayt (as) wana nafasi maalumu baina ya wananchi Waislamu wa Afghanistan, bila shaka vizuizi vya kufanya maombolezo haviwezi kukubaliwa na jamii ya Kiislamu ya Afghanistan.

 

Takwa la Baraza la Maulamaa wa Kishia wa Afghanistan kwa waombolezaji wote wa nchi hiyo la kuratibu na kushirikiana na vikosi vya Taliban katika utekelezaji wa maombolezo ya Muharram na Ashura linaonyesha kuwa Mashia wanafuata sheria kikamilifu na wanatarajia Taliban kuondoa vizuzi vilivyotangazwa kwa kutumia vikosi vya wananchi katika kudhamini usalama wa maombolezo ya Muharram.

Seyyid Issa Mazari Husseini mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema:

Watu wa Afghanistan wako tayari kushirikiana na Taliban katika uwanja wa kudhamini usalama wa maombolezo ya Muharram ili kila mtu aweze kushiriki katika maombolezo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s.) na kuondolewa kwa vizingiti vilivyowekwa bila shaka kutakuwa na ufanisi katika kuimarisha nafasi ya kijamii ya Taliban katika jamii ya Afghanistan. Kwa sababu utendaji wa Taliban kawaida umejikita zaidi katiika kuzuia shughuli za kijamii, na hilo halijawa na ujumbe mzuri kwa jamii ya Afghanistan.

Matamshi ya Zabihullah Mujahid, msemaji wa serikali ya Taliban ya Afghanistan kwamba, Mashia wako huru kuendesha maombolezo ya Muharram na kwamba serikali inaunga mkono uhuru wa kidini, yanakinzana wazi na uamuzi wa kuwekwa baadhi ya vizuizi. Bila shaka, kutangazwa kwa uamuzi mmoja wa Taliban wa uhuru wa kufanya maombolezo ya Muharram kutakuwa na maana ya kuheshimu maoni na itikadi ya jamii ya wengi, yenye kaumu na madhehebu tofauti nchini Afghanistan.