Mauaji ya makusudi dhidi ya raia wa Ghaza wasio na hatia
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni ametangaza kuwa ametoa amri ya kuzingirwa kikamilifu Ukanda wa Ghaza.
Mapigano kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na wanamapambano wa Palestina yalianza Jumamosi na ijapokuwa yalianzishwa na Wapiganaji wa Harakati ya Hamas, lakini hata baadhi ya Wazayuni wanaamini kuwa siasa kandamizi na jinai za Israel ndicho chanzo cha uamuzi wa Hamas wa kuingia vitani. Viongozi wa Hamas pia wanasema kuwa hatua yao hiyo ilikuwa ni ya kujitetea dhidi ya jinai za utawala huo ghasibu hususan kuhusiana na mateka na kushambuliwa Msikiti wa Al-Aqsa, jambo ambalo linaruhusiwa kisheria.
Utawala wa Kizayuni ambao umeshangazwa na kupigwa butwaa na Kimbunga cha Al Aqsa hivi sasa unatekeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Jeshi la utawala huo ghasibu limetangaza rasmi kuwa limedondosha zaidi ya tani 1,000 za milipuko kwenye ukanda huo. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza, Wapalestina 496 wakiwemo watoto 150 na zaidi ya wanawake 200 wameuawa katika mashambulizi hayo ya kijina huko Ghaza. vilevile Wapalestina 2,751 wakiwemo watoto 244 na wanawake 151 wamejeruhiwa. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu pia imeripoti kuwa, wakaazi 123,538 wa Ukanda wa Gaza wamekimbia makazi yao kutokana na mashambulio hayo ya mabomu. Shirika la habari la Palestina limeripoti kuwa sasa utawala wa Kizayuni unashambulia kwa makusudi vituo vya makazi na vilevile kambi mahsusi za wakimbizi huko Ghaza.
Pamoja na hayo, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni, Yoav Gallant ametangaza kuwa ametoa agizo la kuzingirwa kikamilifu eneo la Ghaza na kuongeza kuwa kwa mujibu wa amri hiyo, maji, umeme na mafuta hayapaswi kuingia katika eneo hilo. Agizo hilo la Waziri wa Vita wa Israeli lina nukta kadhaa muhimu.
Nukta ya kwanza ni kwamba Tel Aviv inalipiza kisasi cha kushtukizwa na kushindwa kwake kubaya zaidi kijeshi katika historia yake kwa kuua kwa makusudi raia wa Gaza, wakiwemo wanawake na watoto. Hatua hiyo ni ishara nyingine ya kukata tamaa na kushindwa kwake katika medani ya katika makabiliano na wapiganaji wa Palestina.
Nukta ya pili ni kuwa, utawala wa Kizayuni unajaribu kutuliza na kuponya machungu makubwa ya kushindwa huko kihistoria kwa kuua kiholela raia wa Ghaza. Lakini bila shaka maumivu hayo hayatapungua kwa sababu itibari ya kijeshi ya utawala huo wa kibaguzi imeharibiwa na Kimbunga cha Al-Aqsa. Katika ripoti yake kuhusu operesheni za jeshi la muqawama wa Palestina dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni, jarida la The Guardian la Uingereza limeandika kuwa Shambulio la kushtukiza la Hamas dhidi ya Israel litakumbukwa kuwa pigo la karne dhidi ya taasisi za kijasusi na kiusalama za utawala huo.
Nukta ya tatu ni kwamba Ghaza, yenye eneo dogo la kilomita mraba 365, imekuwa chini ya mzingiro kamili kwa miaka 16, hivyo kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani, lakini pamoja na hayo haijakubali kudhalilishwa na watendajinai wa Kizayuni, ambapo siku ya Jumamosi, eneo hilo dogo na lenye suhula chache kabisa lilitekeleza operesheni ya kishujaa na kuutwisha utawala huo kushindwa kukubwa zaidi ambako kulikuwa hakujawahi kushuhudiwa tena katika historia yake iliyojaa jinai na mauaji ya kigaidi. Kuzingirwa na kutekelezwa mauji ya kigaidi hakutawapelekea Wapalestina kusalimu amri, bali kutaibua kushindwa kwingine kwa Wazayuni, leo na katika siku zijazo.
Nukta ya nne; huenda nchi ambazo zimekuwa zikieleza wasiwasi wao kuhusu usalama na hali ya utawala wa Kizayuni tangu Jumamosi iliyopita, haziyaoni mauaji ya hivi sasa dhidi ya raia wa Ghaza wasio na hatia, hususan wanawake na watoto, au zinayaona lakini mauaji hayo huenda hayana nafasi kabisa katika tafsiri yao kuhusu haki za binadamu. Lau madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu yangechukizwa na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na kuchukua hatua dhidi ya utawala huo, bila shaka hujuma kama hiyo ya kijinai dhidi ya watu wasio na hatia isingetokea.