Wapalestina waandamana Ukingo wa Magharibi kuwaunga mkono wenzao wa Ghaza
Raia wa Palestina wamefanya maadnamano katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuonyesha uungaji mkono wao kwa wenzao wa Ukanda wa Ghaza sambamba na kuyaunga mkono makundi ya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Wanamapambano wa Palestina tangu Jumamosi iliyopita wameanzisha oparesheni kubwa kwa jina la " Kimbunga cha Al Aqsa"; ambayo hadi sasa imepelekea kuangamizwa Wazayuni zaidi ya elfu moja na kujeruhiwa wengine zaidi ya elfu mbili.
Ripoti ya shirika la habari la Shehab inaeleza kuwa, sambamba na kuongezeka idadi ya mashahidi waliouliwa katika mashambulizi ya utawala gaidi wa Kizayuni, raia wa Palestina leo asubuhi wameandamana katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi katika kuunga mkono oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa iliyotekelezwa na makundi ya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Wakati huo huo, wanamuqawama katika mji wa Nablus wameandamana kwa kutumia magari na pikipiki mbele ya vituo vya ukaguzi vya utawala wa Kizayuni katika kuwaunga mkono na kuonyesha mshikamano wao na wenzao wa Ukanda wa Ghaza.
Katika kambi ya wakimbizi ya Jenin pia, misikiti imekuwa ikitoa wito wa kufanyika maandamano ili kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.
Hii ni katika hali ambayo vyombo vya Palestina pia vimetangaza kuwa, wakazi wa Kipalestina huko Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nao wameandamana katika mitaa mbalimbali ya mji huo kupinga mashambulizi ya kinyama ya utawala gaidi wa Kizayuni.