Wazayuni waendeleza jinai dhidi ya Wapalestina, jamii ya kimataifa yaonya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103470-wazayuni_waendeleza_jinai_dhidi_ya_wapalestina_jamii_ya_kimataifa_yaonya
Taasisi na asasi mbalimbali za kimataifa zinaendelea kulaani mpango wa kikatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu wananchi wa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2023 10:06 UTC
  • Wazayuni waendeleza jinai dhidi ya Wapalestina, jamii ya kimataifa yaonya

Taasisi na asasi mbalimbali za kimataifa zinaendelea kulaani mpango wa kikatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu wananchi wa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Tishio la utawala wa Kizayuni la kuwahamisha kwa nguvu na kuzidi kuwaua kwa umati wananchi wa kaskazini mwa Ghaza limetolewa katika hali ambayo baadhi ya taarifa zinasema kuwa, ziara ya hivi karibuni ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani katika nchi za Kiarabu lilikuwa ni ya kujaribu kuzishawishi nchi hizo ziwapokee Wapalestina wa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Duru mbalimbali za kieneo na za kimataifa hata zile zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni zimelaani mpango huo na kusema kuwa ni jinai na lazima usimamishwe mara moja.

Wazayuni hawatoweza kuteteresha imani ya Wapalestina kwa jinai zao kama hizi

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, hata vita navyo vina sheria zake na hivi sasa hali ya Ukanda wa Ghaza imefikia kiwango cha hatari.

Amesema, mfumo wote wa matibabu katika Ukanda wa Ghaza umekaribia kusambaratika kikamilifu na kwamba maeneo ya kuhifadhia maiti hayana uwezo tena wa kupokea maiti wote wanaouliwa kwenye mashambulio ya Israel.

Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limesema kuwa, mpango wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza utasababisha janga kubwa la afya na haiwezekani kabisa kuzihamisha hospitali za kaskazini mwa Ghaza na kuzipeleka sehemu nyingine.

Siku watoto watakapoulizwa, ni kwa kosa gani mumeuawa?

 

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu nalo limetangaza kuwa, mashirika ya kimataifa ya misaada yanashindwa kuwasaidia wananchi wa Ghaza wanaohitajia mno misaada ya kigeni, kutokana na mashambulio ya Israel na kuendelea kuzingirwa kila upande ukanda huo.

Takwimu zinaonesha kuwa hadi hivi sasa zaidi ya Wapalestina 2,000 wameshauawa shahidi na zaidi ya 7,000 wengine wameshajeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha jinai zao Jumamosi iliyopita. 600 kati ya Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulio ya kikatili ya Israel, ni watoto wadogo.