Kuongezeka wimbi la Wazayuni wanaokimbia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel)
Ingawa wimbi la kuhajiri Wazayuni kutoka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kuelekea katika nchi walikotoka lilianza huko nyuma, lakini wimbi hilo limeshika kasi sasa baada ya kuanza vita dhidi ya Gaza.
Siku 63 za vita vilivyoanzisha na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza zimepita sasa. Moja ya matokeo makuu ya vita vya utawala wa Kizayuni ni kushadidi wimbi la kugura walowezi na Wazayuni kutoka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kurejea walikotoka. Ripoti za vyombo vya habari vya Kizayuni zinaeleza kuwa, watu walioondoka kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu kuanza oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa imefika laki tano. Nukta nyingine muhimu ni kuwa, hakuna mtu yoyote kati ya hao walioondoka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambaye amerejea tena katika ardhi hizo.
Wimbi hili la kuhama lilianza kabla ya kuanza vita vya Gaza Oktoba 7 mwaka huu. Idara ya Huduma ya Uhamiaji ya Ureno imetangaza kuwa raia 21 kutoka katika Israel wametuma maombi ya kupatiwa uraia wa nchi hiyo tangu mwanzoni mwaka huu. Takwimu zinaonyesha kuwa watu hao wamewekwa katika safu ya kwanza ya watu walioomba kupewa uraia wa Ureno ikilinganishwa na raia wa nchi nyingine.
Kabla ya kuanza Kimbunga cha Al Aqsa, sababu kuu ya kushuhudiwa hamahama hii ya walowezi kutoka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ilikuwa matatizo na changamoto nyingi za kiuchumi. Hata hivyo baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa, masuala ya usalama pia yameongezeka sana. Vita vimesababisha ukosefu wa amani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hasa ikizingatiwa kuwa, matatizo ya kiuchumi pia yameongezeka pakubwa hususan ukitilia maanani kuwa suala la ukosefu wa ajira huko Israel limeshadidi zaidi.
Hali ya kiuchumi imekuwa mbaya sana baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa kiasi kwamba, idadi ya watu wasio na ajira katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu inakaribia milioni moja. Wizara ya Kazi ya utawala wa Kizayuni imetangaza katika taarifa yake kwamba hadi kufikia siku ya 26 baada ya kuanza oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa Wazayuni 760,000 halipoteza ajira na kazi zao. Hapana shaka yoyote kwamba takwimu hizi zimeongezeka. Sasa, pamoja na masuala ya kiuchumi na kimaisha, usalama bandia wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni pia umefichuliwa; ambapo wakaazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu sio tu kwamba hawafurahii ustawi wa kiuchumi, bali pia wameazimia kuikimbia Israel wakihofia kushambuliwa wakati wowote na makombora ya wapigania uhuru wa Palestina. Mojawapo ya maneno yanayovuma na kuongoza katika kitengo cha search (tafuta) cha Google kuhusu raia wa Israeli, ni neno "kuondoka Israel".
Suala jingine ni kuwa, licha ya suala la kkuhajiri na kuhama, wahamiaji Wazayuni wanajaribu kila njia ili kupewa uraia wa nchi nyingine. Kwa msingi huo, moja ya daghadagha kubwa inayowasumbua sasa raia wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni kupata nchi ya nje ambayo itawapatia uraia na pasi yza kusafiria. Zaidi ya yote, wahamiaji hawa wanachagua nchi za Ulaya kama maeneo yao ya kuhajiri. Takwimu rasmi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zinaonyesha kuwa, kiwango cha maombi ya raia wa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kupewa uraia wa Ureno, Ujerumani na Poland kimeongezeka. Ofisi ya Umoja wa Ulaya huko Tel Aviv imekiri kuwa, kunashuhudiwa mchakato unaoongezeka kila siku wa raia wa utawala wa Kizayuni wanaohajiri na kuhamia katika nchi wanachama wa umoja huo.
Kwa kuzingatia hali hii, serikali ya sasa na ya baadaye ya utawala wa Kizayuni wa Israel inapasa kufikiria juu ya mpango wa kuzuia wimbi hili la uhamiaji na njia za kuwarejesha; mpango ambao ni vigumu kufanikiwa katika kipindi kifupi.