Hali ya zama za mwisho ya Ukanda wa Gaza
Mashambulizi makali ya ndege za kivita ya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza yaliendelea jana Jumanne kwa masaa kadhaa.
Karibu siku 70 zimepita sasa tangu kutekelezwa oparesheni ya wanamuqawama wa Palestina ya Kimbunga cha al Aqsa na ndege za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni kushambulia makazi ya raia khususan kambi na maeneo yanayowahifadhi wakimbizi wa Palestina huko Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza jana asubuhi ilitangaza kuwa: "Wazayuni wanashambulia hospitali, madaktari na wauguzi; na karibu majeruhi elfu nane wanahitaji kufanyiwa upasuaji haraka iwezekanavyo."
Maafisa wa tiba wa Gaza wameeleza kuwa, tangu Oktoba 7 mwaka huu Wapalestina 18,000 wameuliwa shahidi na zaidi ya wengine 49,229 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya kikatili ya anga na nchi kavu dhidi ya eneo hilo. Takwimu hizi zinazidi kuongezeka hasa kutokana na kushtadi mashambulizi ya utawala wa Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yameitaja hali ya Gaza kuwa ya maafa katika kalibu ya mashambulizi ya kinyama ya kila uchao ya utawala wa Kizayuni; na kusema: Nusu ya jamii ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na njaa ambapo gharama ya kila gunia moja la unga wa ngano pia imeongezeka na kufikia dola 95 kufuatia vita katika eneo hilo.
Michael Fakhri Ripota wa Umoja wa Mataifa anayehusika na ripoti kuhusu haki ya chakula amesisitiza katika mahojiano na televisheni ya al Jazeera kuwa:" Watu zaidi ya milioni mbili na laki tatu wanakabiliwa na njaa katika Ukanda wa Gaza."
Wakati huo huo Phillipe Lazarini Kamishna Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) pia juzi alisisitiza kuwa: Israel inafanya kila iwezalo kuwahamisha kwa lazima na kwa umati raia wa Palestina huko Gaza. Ameongeza kuwa, kuna udharura wa kusimamishwa vita ili kusitisha jahanam iliyoanzishwa huko Ukanda wa Gaza. Unrwa na muundo mzima wa Ukanda wa Gaza karibuni hivi utasambaratika; na hii inamaanisha khiyana na kutojali jamii ya kimataifa kuhusu hali ya raia wa Ukanda wa Gaza.
Marekani ni miongoni mwa nchi ambazo miaka kadhaa ya karibuni zimeunga mkono pakubwa jinai za Wazayuni; na hivyo kuutia kiburi utawala huo haramu cha kutekeleza jinai zake za kutisha dhidi ya Wapalestina.
Wakati huo huo kura ya veto ya majuzi iliyopigwa na Marekani dhidi ya azimio lililotaka kusitishwa vita Ukanda wa Gaza inaonyesha kuwa huenda Marekani ikawa inataka kuendelezwa vita Gaza kuliko utawala wa Israel. Tarehe 8 mwezi huu wa Disemba ililipiga kura ya veto dhidi ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa mara moja vita huko Gaza. Uingereza ilijizuia kupiga kura, na wanachama wengine 13 wa Baraza la Usalama walipiga kura kuunga mkono azimio hilo.
Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imethibitisha kuwasilisha kwa Israel shehena ya makombora 14,000 ambayo ni moja ya silaha muhimu zinazotumiwa na jeshi la utawala huo katika operesheni za nchi kavu.
Mark Glenn mchambuzi na mwandishi wa Kimarekani anaamini kuwa tofauti iliyopo kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni ni kama tofauti kati ya mguu wa kulia na ule wa kushoto wa mtu. Hii ina maana kwamba miguu yote ni sehemu ya mwili mmoja." Akizungumzia uungaji mkono mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Israel Glenn amekumbusha kuwa: Kama Tel Aviv isingepata misaada ya kifedha, kijeshi na kisiasa ya Washington basi utawala huo ungeshambaratika tangu miaka kadhaa iliyopita.
Utawala wa Kizayuni ulipata kipigo kikali katika historia yake ya karibu miaka 70 kufuatia operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha al Aqsa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Taathira za kushindwa utawala wa Kizayuni zimeipekelea Israel kwa ghadhabu na kuweuka kutafuta fidia ya kushindwa kwake mbele ya wanamuqawama wa Palestina; na yanayotokea Gaza leo ni matokeo ya kichaa hicho ambacho Wazayuni wameangukia ndani yake.