Hasara kubwa za Wazayuni katika vita vya Al-Shujaiyya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106168-hasara_kubwa_za_wazayuni_katika_vita_vya_al_shujaiyya
Wazayuni wanajitahidi kuingia katika eneo la Al-Shuja'iyya huko Gaza, huku kukiwa hakuna dalili za kufanikiwa kwao katika eneo hilo.
(last modified 2024-05-29T07:24:47+00:00 )
Dec 19, 2023 01:37 UTC
  • Hasara kubwa za Wazayuni katika vita vya Al-Shujaiyya

Wazayuni wanajitahidi kuingia katika eneo la Al-Shuja'iyya huko Gaza, huku kukiwa hakuna dalili za kufanikiwa kwao katika eneo hilo.

Mwezi wa tatu wa vita vya Gaza pia unapita huku utawala wa Kizayuni ukiwa bado haujafikia malengo yake ya kijeshi, yaani kuachiliwa huru mateka na kuangamizwa kundi la Hamas. Al-Shujaiyya ni mojawapo ya vitongoji vikubwa zaidi katika mji wa Gaza. Jeshi la Israel lilishambulia kitongoji hicho Jumatano iliyopita Desemba 13, lakini likapata pigo kubwa zaidi. Kwa mujibu wa takwimu za Wazayuni, askari jeshi wake 10 kutoka brigedi ya Golani waliangamizwa katika shambulizi hilo, lakini takwimu zisizo rasmi zinaeleza kuangamizwa idadi kubwa zaidi ya askari vamizi wa Kizayuni. Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeandika kjwamba: "Mapigano ya umwagaji damu yanaendelea katika kitongoji cha Al-Shuja'iyyah huko Gaza, na Brigedi ya Golani "inapitia hali ngumu na machungu mengi." Gazeti la Kizayuni la Ma'ariv limeandika kichwa cha habari kinachosema kuhusiana na jambo hilo: "Asubuhi ya machungu." Hizi ndizo zilikuwa habari muhimu za magazeti muhimu ya Kizayuni kuhusiana na mapigano makali na ya kishujaa ya vikosi vya muqawama kaskazini mwa Gaza, yaliyopelekea kuangamizwa askari 10 wakiwemo maafisa wakuu wa jeshi la Israel.

Majeruhi wa askari vamizi

Tunapasa kusema kuwa al-Shuja'iyya ni miongoni mwa maeneo muhimu ya Gaza na mgome nyeti ya idadi kubwa ya vikosi vya Hamas. Wazayuni wanaamini kuwa mahandaki na njia za chini kwa chini za Hamas pia ziko katika eneo hilo. Amir Bu Khobout, mwandishi wa kijeshi wa tovuti ya habari ya lugha ya Kiibrania "Walla" ameandika juu ya umuhimu wa vita vya Al-Shuja'iyya na kusema: "Eneo la Al-Shuja'iyya, lililoko mashariki mwa Gaza linachukuliwa kuwa moja ya maeneo hatari zaidi katika Mashariki ya Kati kwa Tel Aviv, kwa sababu jeshi la utawala huo linakabiliana na hatari ya mashimo, maroketi, visima na mabomu ya kutegwa ardhini yaliyoandaliwa kwa ajili yake na brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina. Ripota wa kijeshi wa gazeti la Ma'ariv pia amesema kwamba majeshi vamizi ya Israel yanakabiliwa na mapigano magumu huko Al Shujaiyyah ambapo Hamas imelenga na kurusha maroketi yasiyohesabika dhidi ya vifaru na magari ya kivita ya Israel katika kitongoji hicho.

Askari wa Kizayuni Gaza

Katika vita vya siku 51 vya mwaka 2014, jeshi la Kizayuni lilinaswa katika kinamasi cha Al-Shujaiyyah na ikabidi liondoke katika kitongoji hicho kutokana na hasara kubwa liliyopata. Tovuti ya habari ya Kizayuni "Walla" ilikumbushia tukio chungu la kushindwa huko na kuandika; 'Mapigano ya siku hiyo yalikuwa magumu sana na hali ya wasiwasi ilitanda katika kikosi hicho baada ya kujeruhiwa kamanda wa brigedi, naibu wake na afisa mwingine. Sitasahau siku hiyo; Tulikuwa tukitafuta miili ya wenzetu katikati ya moto.' Wazayuni wanajaribu kufuta kumbukumbu chungu za mwaka 2014 kwa kutafuta ushindi wa Al-Shuja'iyya katika vita vya hivi sasa, lakini jeraha la Al-Shuja'iyya si tu halitafutika kirahisi, bali linaweza kuwa kali zaidi.

Gazeti la "Haaretz" limeandika: 'Jeshi la Israel halitaweza kufikia malengo yetu ya kisiasa huko Gaza katika muda uliosalia. Licha ya maafa makubwa ya jeshi, hakuna dalili inayoashiria uwezekano wa kushindwa Hamas. Uwezo wetu wa kijeshi unapungua, uwezo wa kiteknolojia na habari za siri hata katika eneo la Al-Shujaiyya haujatufaa kitu na hakuna sababu ya Hamas kuhisi kudhoofika katika mapigano yake na Israel.'