Vikosi vya Yemen vyashambulia tena manowari ya US kwa makombora
Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimefanya shambulio jipya la makombora dhidi ya meli ya kivita ya Marekani katika pwani ya Bahari Nyekundu.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema kuwa meli ya kivita ya Marekani inayojulikana kama USS Gridley ililengwa kwa makombora ya wanamaji wa Yemen hapo jana katika maji ya Bahari Nyekundu.
Amesema shambulio hilo ni muendelezo wa operesheni za kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, ambao wanaendelea kukabiliwa na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na kuungwa mkono kikamilifu na Marekani.
Brigedia Jenerali Yahya Saree ameongeza kuwa, meli za Marekani na Uingereza zinazopita Bahari Nyekundu, Mlango-Bahari wa Bab al-Mandeb, Ghuba ya Aden, na hata katika Bahari ya Arabia ni shabaha halali za vikosi vyake vya kijeshi.
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimesema havitasimamisha mashambulizi yao hadi pale utawala haramu wa Israel utakapokomesha mashambulio yake ya kinyama ya angani na nchi kavu dhidi ya Gaza, ambayo tangu Oktoba 7 hadi sasa yameshateketeza roho za Wapalestina wanaokaribia 27,000.
Wakati huo huo, Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi mapya dhidi ya Yemen, eti kujibu hatua ya jeshi la Yemen ya kuzilenga meli zinazomilikiwa na utawala wa Kizayuni au meli za kibiashara zinazoelekea kwenye bandari za utawala huo ghasibu.
Shirika la habari la SABA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, US na UK zimefanya mashambulizi ya anga mapema leo Alkhamisi katika mkoa wa kaskazini wa Sa’ada na mji wa bandari wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen.