Magaidi wa ISIS wawakata vichwa wachezaji soka na kocha wao
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10909-magaidi_wa_isis_wawakata_vichwa_wachezaji_soka_na_kocha_wao
Magaidi wa kundi la kitakfiri la ISIS au Daesh wamewaua kwa kuwakata vichwa wachezaji soka watatu wa timu ya al Shabab ya Raqaa nchini Syria na kocha wao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2016 23:15 UTC
  • Magaidi wa ISIS wawakata vichwa wachezaji soka na kocha wao

Magaidi wa kundi la kitakfiri la ISIS au Daesh wamewaua kwa kuwakata vichwa wachezaji soka watatu wa timu ya al Shabab ya Raqaa nchini Syria na kocha wao.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Syria SANA, magaidi wakufurishaji kwa ujumla wamewachinja watu watano wakiwemo wachezaji mpira wa mguu waliotambuliwa kama Osama Abu Kuwait, Nihad al-Hussein, Ihssan al-Shawakh na ndugu yake, kocha Ahmad al-Shawakh katika eneo la Dawar al Dalah mjini Raqaa. Wote hao waliuawa kinyama hivi karibuni mbele ya wazee na watoto wao.

Mkuu wa Idara ya Michezo ya Syria Muafak Joma'a amelaani vikali jinai hiyo ya ISIS na kuelezea masikitiko yake kuwa limekuwa jambo la kawaida kwa ISIS kutenda jinai kama hizo.

Mji wa Raqaa ulikaliwa kwa mabavu na ISIS mwaka 2013 na ukawa mji mkuu wa kundi hilo la kigaidi nchini Syria mwaka 2014.

Magaidi wa ISIS awali walipata mafunzo kutoka Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA mwaka 2012 nchini Jordan kwa lengo la kuiangusha serikali ya Syria lakini hawajafanikiwa katika njama hizo. Magaidi hao wamekuwa wakishikilia sehemu kubwa za Iraq, Syria na Libya lakini katika siku za hivi karibuni wamepata pigo kubwa kuotoka majeshi ya nchi hizo na wamepoteza ardhi nyingi walizokuwa wameziteka. Magaidi wa ISIS hutekeleza jinai za kuogofya dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni, Wakristo na pia makabila ya walio wachache kama vile Wakurdi na Waizadi.

Mapigano nchini Syria yalianza Machi 2011 na serikali ya Damascaus inalaumu Marekani na waitifaki wake katika eneo hasa Saudia Arabia, Qatar, Uturuki na Utawala haramu wa Israel kuwa ndio waungaji mkono wa makundi ya kigaidi nchini humo. Vita vya Syria hadi sasa vimepelekea karibu watu nusu milioni kuuawa na karibu nusu ya watu wote milioni 23 nchini humo kulazimika kukimbia makazi yao.