OIC yataka kukomeshwa jinai, uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa mwito kusitishwa mara moja uvamizi na hujuma za kijeshi za utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza.
Mwito huo umetolewa na Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) waliokutana mjini Jeddah, Saudi Arabia katika taarifa yao ya mwisho ambapo wametaka kusitishwa kikamilifu na bila masharti uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu pia wametaka kufunguliwa upya kwa vivuko vya mpakani ili kupokea misaada ya haraka ya kibinadamu huko Gaza bila ya vikwazo.
Taarifa hiyo pia imeonya kuhusu hatari itakayotokana na kuendelea jinai ya mauaji ya umati na mauaji ya kimbari huko Gaza.
Mwishoni mwa taarifa hii, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo na jamiii ya kimataifa ili kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni ukomesha mashambulizi dhidi ya Gaza.
Mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa OIC ulifanyika mjini Jeddah Saudi Arabia jana Jumanne kwa shabaha ya kujadili hali ya Gaza.
Hapo kabla pia, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ilifanya kikao cha dharura cha kamati yake ya utendaji katika ngazi ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama huko Jeddah, Saudi Arabia, ili kuhakiki matukio ya hali ya Gaza kikao ambacho kilifanyika Oktoba 18, 2023.