Kusambaratishwa mtandao mwingine wa kijasusi wa Israel huko Uturuki
Utawala wa kibaguzi wa Israel bado unaendeleza operesheni zake za kijasusi dhidi ya Waislamu wa Uturuki.
Kuhusiana na jambo hilo, Idara ya Upelelezi ya Uturuki imetangaza kuwa imegundua na kusambaratisha mtandao mwingine wa watu 7 waliokuwa wakifanya shughuli za kijasusi nchini humo chini ya shirika la kijasusi la Kizayuni (Mossad). Vyombo vya habari vya Ankara pia vimetangaza kuwa Idara ya Upelelezi ya Uturuki imewakamata watu 7 walipokuwa wakiuza taarifa kwa shirika hilo la ujasusi la utawala haramu wa Israel. Katika hali ambayo Uturuki bado inaendelea kuuzia nishati na bidhaa muhimu utawala ghasibu wa Israel na uhusiano wa pande hizo mbili unazidi kuboreka, kuwepo mitandao mbalimbali ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni nchini humo kunatia wasiwasi na ni suala la kupewa umuhimu.
Kwa kuzingatia kufanyika operesheni nyingi za kijasusi za utawala wa Kizayuni nchini Uturuki, inaonekana kuwa serikali ya Ankara haiweki wazi wala kutangaza baadhi ya mitandao ya kijasusi ya Israel nchini humo. Kwa kutilia maanani shughuli nyingi za ujasusi za Israel nchini Uturuki, tunaweza kusema kwa yakini kuwa shughuli hizo katika miji tofauti ya Uturuki hazipaswi kuchukuliwa kuwa suala la kawaida.
Kukiri uwepo wa majasusi wa Israel nchini Uturuki kunaonyesha kuwa, si tu raia wa nchi za Kiislamu nchini Uturuki ndio walengwa wa shughuli za ujasusi za Mossad, bali kama ilivyo katika nchi zote za Kiislamu, serikali na watu wa Uturuki pia wanakabiliana na vitisho hivyo vya utawala haramu wa Kizayuni. Kwa mujibu wa ripoti za siri za wanasiasa wastaafu wa Uturuki na viongozi wa Marekani, viongozi wa Ankara wanapaswa kuzingatia zaidi ukweli kwamba Uturuki ni miongoni mwa walengwa wakuu wa mashirika ya kijasusi duniani hususan ya utawala wa Kizayuni.

Katika muktadha huo, tunaweza kuashiria kauli ya "Madeleine Albright", Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani na ambaye pia alikuwa mtaalamu wa siasa za Magharibi. Alisema kwa uwazi kuwa: "Uturuki ni nchi kubwa mno kubaki kuwa ni ya Waturuki tu". Kwa hakika, mwanasiasa huyo wa kidemokrat wa Marekani alizungumza kwa uwazi miongo miwili iliyopita kuhusu uwezekano wa kugawanywa ardhi ya Uturuki na kuwa vipande vya nchi kadhaa. Katika hali hiyo, hatupaswi kupuuza ukweli kwamba serikali za Magharibi zikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni zinafanya jitihada za kila namna ili kuigawa Uturuki, na zinatumia kila fursa ili kupiga hatua moja mbele katika uwanja huo.
Licha ya hayo, inaonekana kwamba maafisa wa serikali ya Raus Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki wanajaribu kuimarisha uhusiano na maadui wa kujitawala na umoja wa ardhi ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia mchakato wa sasa, tunapaswa kusisitiza kwamba hii si mara ya kwanza kukamatwa kundi la majasusi 7 wa Mossad nchini Uturuki. Huko nyuma na katika kipindi cha mwaka uliopita makundi mengi ya kijasusi ya Israeli yamegunduliwa na kunaswa nchini Uturuki. Awali, Ankara iligundua na kutangaza hadharani visa vingi vya operesheni chafu, hususan shughuli za kijasusi za utawala wa Kizayuni nchini humo. Ni wazi kuwa huo ni mtandao wa saba wa kijasusi wa Israeli kugunduliwa na kusambaratishwa nchini Uturuki katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Kufichuliwa na kusambaratishwa pamoja na kutiwa mbaroni majasusi wa utawala wa Kizayuni kunaonyesha kuwa utawala huo haramu umejiimarisha sana huko Uturuki na unafanya jitihada zake zote ili kufikia malengo yake ya kuiangamiza nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa nchi muhimu za Kiislamu. Kwa kuwa wazi suala hilo, tunaweza kusema kuwa utawala wa Kizayuni, kinyume na mitazamo ya wanasiasa wengi wa Kiislamu, unafanya kila uwezalo ili kuzidhuru jamii za Kiislamu.
Kwa kuzingatia suala hilo, siasa za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya madola na mataifa ya Kiislamu hazipaswi kupuuzwa. Kwa hakika harakati za utawala wa Kizayuni zinaratibiwa na kutekelezwa kwa kuzingatia matakwa na maslahi ya nchi za Magharibi, na ujasusi wa mara kwa mara wa maajenti wa Israel nchini Uturuki unaonyesha kuwa, mipango na siasa za kuigawa Uturuki bado ziko kwenye ajenda ya madola ya Magharibi na uhasama na vilevile uadui unaochochewa kati ya Uturuki na nchi jirani zake ni mojawapo tu ya mbinu ambazo zinapewa kipaumbele na madola hayo ya kibeberu.