Wafanyakazi wa UNRWA waliteswa ili wakiri uwongo dhidi ya Hamas
Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina (UNRWA) limekusanya ripoti kuhusu jinai za Tel Aviv dhidi ya haki za binadamu katika vita dhidi ya Ukanda wa Gaza, na kufichua "mateso na dhuluma" walizofanyiwa wafanyakazi wa shirika hilo katika jela za utawala ghasibu wa Israel ili wakiri tuhuma bandia dhidi ya Hamas.
Shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, Shirika la UNRWA limetangaza kuwa baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela za utawala wa Israel unaotenda mauaji ya kimbari wameeleza kuwa walikuwa chini ya mashinikizo ya maafisa wa Israel ambapo iliwalazimu kusema uwongo kwamba shirika hilo la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina lina uhusiano na harakati ya Hamas na kwamba, wafanyakazi wake walishiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7.
Wakati huo huo shirika la habari la Reuters liliipata ripoti ya UNRWA iliyowaslishwa mwezi Februari mwaka huu katika kujibu tuhuma za Tel Aviv dhidi ya UNRWA na kumnukuu Juliette Touma Mkurugenzi wa Mawasiliano wa UNRWA na kuandika: Shirika hilo linapanga kukabidhi kwa mashirika, ndani na nje ya Umoja wa Mataifa ambayo yana utaalamu wa kuweka kumbukumbu juu ya ukiukwaji wowote wa haki za binadamu.
Juliette Touma ameeleza kuwa kupigwa, kuzamishwa katika maji bandia, vitisho vya kuwadhuru wanafamilia ni miongoni mwa mateso yanayofanyiwa wafanyakazi wa UNRWA na utawala wa Israel na kusisitiza kuwa uchunguzi mtawalia unapasa kufanywa vita vitakapomalizika ili kurekodi visa vyote vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Miezi kadhaa iliyopita utawala wa Kizayuni uliwatuhumu wafanyakazi 12 wa shirika la UNRWA katika Ukanda wa Gaza kuwa walishirikiana na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kutekeleza oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa; na kwa kisingizio hicho hicho, nchi 18 na Umoja wa Ulaya zilisitisha misaada yao ya kifedha kwa shirika hilo bila ya kuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha tuhuma hizo za Tel Aviv.