Waliouawa shahidi Gaza wakaribia 32,000; Israel yaendeleza mashambulizi ya kinyama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i109350-waliouawa_shahidi_gaza_wakaribia_32_000_israel_yaendeleza_mashambulizi_ya_kinyama
Duru za afya katika Ukanda wa Gaza huko Palestina zimetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kufuatia mashambulio ya kinyama ya Israel imekaribia 32,000.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Mar 11, 2024 00:50 UTC
  • Waliouawa shahidi Gaza wakaribia 32,000; Israel yaendeleza mashambulizi ya kinyama

Duru za afya katika Ukanda wa Gaza huko Palestina zimetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kufuatia mashambulio ya kinyama ya Israel imekaribia 32,000.

 Ripoti zinaeleza kuwa, wakati vita angamizi vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza vimeingia mwezi wa sita sasa Wapalestina 31,450 wameshauawa shahidi na 72,654 wamejeruhiwa.

Kwa upande mwingine, na katika msimamo wa karibuni zaidi aliotoa kuhusu Gaza, Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili, amesisitiza juu ya kuwaunga mkono wakazi wanaodhulumiwa wa eneo hilo.

Huku akiashiria mashambulizi yasiyokoma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya mji ya Rafah ambayo yamesababisha mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na kujeruhiwa, Sheikh Al Khalili amesema, "tunashangazwa na kimya cha nchi majirani kuhusiana na jinai hizi; kwamba kwa nini hazichukui hatua yoyote kuwasaidia wanaodhulumiwa?"

Mufti wa Oman, Samahat Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili

 

Kabla ya hapo, Mufti wa Oman alieleza kuwa hali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu imezidi kuwa mbaya na dhulma imefikia kiwango cha kutisha na akaongezea kwa kusema, watu wanaopambama na wanaodhulumiwa wa Palestina wanataabika kwa njaa, lakini ndugu zao wanawasaliti kwa kumsaidia adui na kumfungulia njia ya kupitishia bidhaa zake.

Katika upande mwingine, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa mwito kusitishwa mara moja uvamizi na hujuma za kijeshi za utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza.

Mwito huo ulitolewa na Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) waliokutana hivi karibuni mjini Jeddah, Saudi Arabia katika taarifa yao ya mwisho ambapo wametaka kusitishwa kikamilifu na bila masharti uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.