Wapalestina waanza mfungo wa Ramadhani katika hali ya vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i109354-wapalestina_waanza_mfungo_wa_ramadhani_katika_hali_ya_vita
Wapalestina wameanza mfungo wa mwezi wa Ramadhani katika hali ya huzuni na hatua zilizoimarishwa za usalama na polisi ya utawala haramu wa Israel. Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya kupatikana muafaka wa kusitishwa mapigano yamekwama.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Mar 11, 2024 00:51 UTC
  • Wapalestina waanza mfungo wa Ramadhani katika hali ya vita

Wapalestina wameanza mfungo wa mwezi wa Ramadhani katika hali ya huzuni na hatua zilizoimarishwa za usalama na polisi ya utawala haramu wa Israel. Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya kupatikana muafaka wa kusitishwa mapigano yamekwama.

Maelfu ya polisi wamewekwa katika mitaa ya Mji Mkongwe wa Baytul-Muqaddas ambako maelfu ya waumini wanatarajiwa kila siku kufika katika eneo la Msikiti wa Al Aqsa, mojawapo ya maeneo matakatifu zaidi katika dini ya Kiislamu.

Mashambulizi ya mfululizo ya Israel huko Gaza yamesababisha wasiwasi mkubwa kote duniani wakati hatari inayoongezeka ya njaa.

Matumaini ya kusitishwa mapigano, ambayo yangeruhusu mfungo wa Ramadhan kumalizika kwa amani na kuwezesha kuwachiwa kwa angalau baadhi ya mateka 134 wa Israel wanaoshikiliwa Gaza, yanaonekana kudidimia, baada ya mazungumzo ya mjini Cairo kukwama.

 

Hivi majuzi Philippe Lazzarini Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) alisema kuwa, baa la njaa kali lililozagaa katika Ukanda wa Gaza linaweza kuepukwa ikiwa misaada itaruhusiwa kuingizwa katika eneo hilo.

Lazzarini ameeleza bayana kuwa janga hilo ni la kutengenezwa na watu akikumbusha kuwa ulimwengu uliahidi kutoruhusu baa la njaa litokee tena na akaongezea kwa kusema, janga la njaa huko Gaza lingali linaweza kuepukwa kupitia utashi wa kweli wa kisiasa utakaowezesha kufunguliwa njia na kutoa ulinzi ili kufikisha misaada athirifu.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeshtakiwa kufanya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ). Uamuzi wa muda uliotolewa na mahakama hiyo mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya kimbari na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu inatolewa na kufikishwa kwa raia huko Gaza.