Marekani ina wasiwasi wa Israel kushindwa katika vita vya Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112068-marekani_ina_wasiwasi_wa_israel_kushindwa_katika_vita_vya_ghaza
Gazeti la mtandaoni la Politico limeeleza katika ripoti yake kwamba, Marekani ina wasiwasi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushindwa katika vita vya Ghaza.
(last modified 2024-05-23T00:48:42+00:00 )
May 23, 2024 00:48 UTC
  • Marekani ina wasiwasi wa Israel kushindwa katika vita vya Ghaza

Gazeti la mtandaoni la Politico limeeleza katika ripoti yake kwamba, Marekani ina wasiwasi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushindwa katika vita vya Ghaza.

Katika ripoti yake hiyo, Politico limeeleza kuwa, viongozi wa Marekani wanakiri kwamba utawala wa Kizayuni umeweza kuangamiza sehemu ndogo tu ya uwezo wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS katika vita, na Ikulu ya White House inahofia utawala huo kushindwa katika vita hivyo vya Ghaza.

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mkakati wa utawala wa Kizayuni wa Ghaza unaelekea kushindwa na unafungua njia ya kuibuka tena Hamas; kauli ambayo haikuwahi kusikika mwanzoni mwa vita hadi hivi majuzi.

Gazeti hilo la Marekani limeendeleza kueleza katika ripoti yake kwamba: mashirika ya intelijensia ya Marekani yanaamini kuwa ni 30-35% tu ya wapiganaji wa Hamas wameuawa katika vita vya Ghaza, na karibu 65% ya mahandaki ya chini ya ardhi Muqawama wa Palestina yamebaki salama hadi sasa.

Ripoti ya Politico imebainisha kuwa, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, Israel imeshindwa kudhibiti maeneo Ghaza iliyoyakalia hapo kabla; imewafanya walimwengu wasimame dhidi yake kwa mashambulizi makubwa kupindukia uliyofanya na kwa kuzuia misaada ya kutosha ya kibinadamu isiwafikie watu wa Ghaza na wakati huohuo imeshindwa kuizuia Hamas isiandae wapiganaji wengine wapya.

Politico imenukuu duru za kuaminika za serikali ya Marekani zikieleza kwamba Hamas imepoteza si zaidi ya 35% ya vikosi vyake katika vita vya Ghaza, lakini wakati huohuo imeandaa maelfu ya wanachama wengine wapya.

Tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023, Wamarekani wamekuwa muda wote wakijiepusha kufanya ukosoaji wowote dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.../