Jinai ya Nuseirat na kuendelea kukashifika kimaadili Marekani na Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112782-jinai_ya_nuseirat_na_kuendelea_kukashifika_kimaadili_marekani_na_wazayuni
Jinai iliyofanywa na Marekani na Wazayuni kwenye kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Nuseirat katika Ukanda wa Ghaza inadhihirisha zaidi, kuliko jambo jengine lolote, kuendelea kukashifika na kuaibika kimaadili Washington na Tel Aviv.
(last modified 2026-05-02T17:46:50+00:00 )
Jun 10, 2024 23:02 UTC
  • Jinai ya Nuseirat na kuendelea kukashifika kimaadili Marekani na Wazayuni

Jinai iliyofanywa na Marekani na Wazayuni kwenye kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Nuseirat katika Ukanda wa Ghaza inadhihirisha zaidi, kuliko jambo jengine lolote, kuendelea kukashifika na kuaibika kimaadili Washington na Tel Aviv.

Siku ya Jumamosi tarehe 8 Juni, jeshi la utawala wa Kizayuni liliendeleza jinai zake za kinyama dhidi ya raia wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza, kwa kufanya shambulio la kiwendawazimu dhidi ya kambi ya Nuseirat katikati mwa Ghaza kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani.
Duru za tiba za Palestina zimetangaza kuwa, idadi ya waliouawa shahidi katika jinai hiyo iliyofanywa na adui Mzayuni huko Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Ghaza imefikia watu 274 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia watu 698, ambapo baadhi yao wako mahututi na wengine wengi wangali wako chini ya kifusi.
Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza pia kuwa: jeshi la utawala wa Kizayuni lilishambulia kwa makombora na mabomu nyumba 89 na majengo ya makazi ya watu wakati wa jinai yake ya Jumamosi huko Nuseirat.

Wakati wa shambulio hilo la kikatili na kinyama dhidi ya raia katika kambi ya Nuseirat, utawala ghasibu wa Kizayuni uliwakomboa mateka wanne Waisrael, ingawa hilo liliweza kufanywa kwa msaada wa vyombo vya intelijensia na kijasusi vya Marekani na Magharibi na wa vikosi vya mamluki, ambavyo viliwapa ulinzi maghasibu wa Kizayuni kwa kutumia lori lililobeba misaada ya kibinadamu.

Baada ya kufanya jinai hiyo Wazayuni walisherehekea, lakini wachambuzi wengi hususan wachambuzi wa Kizayuni wanaamini kuwa, kukombolewa mateka wanne baada ya miezi minane ya vita, tena kwa gharama ya kuua na kujeruhi Wapalestina wapatao elfu moja hakuwezi kuhesabiwa kuwa ni ushindi.
 
Wataalamu wa Kizayuni wanaitakidi kuwa, matokeo ya operesheni ya kijeshi iliyofanywa na Israel hayawezi kwa namna yoyote ile kuchukuliwa kuwa ushindi wa kistratejia na kimkakati, ambao unaweza kubadilisha sura ya vita au kuboresha hali ya Israel.
Yossi Fartar, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Kizayuni, ameandika makala iliyochapishwa na gazeti la Kiebrania la Haaretz akieleza kwamba Netanyahu aliharakisha kupiga picha na mateka wa Israel waliokombolewa, lakini kukombolewa mateka hao hakuwezi kuinasua Israel kwenye kinamasi cha matope ilichokwama ndani yake.

 

Fartar ameendelea kuandika kuwa, bila kupoteza muda, Netanyahu alielekea hospitali ili kuzungumza na mateka hao na kupiga nao picha ya ukumbusho, ilhali hakuwashughulikia wala kuwajali mateka walioachiliwa katika mchakato wa kubadilishana mateka mwezi Novemba wala familia za Waisrael waliouawa.

 
Baadhi ya wachambuzi wa Kizayuni wameashiria nukta moja, nayo ni kwamba, mauaji ya Jumamosi kwenye kambi ya Nuseirat yamewadhihirishia kwa mara nyingine tena walimwengu sura na dhati halisi ya kikatili ya Israel; na kwa sababu hiyo, yameufanya utawala huo utengwe zaidi katika ngazi ya kimataifa, hasa kwa kuzingatia kwamba mauaji hayo yalitokea siku moja tu baada ya jina la Israel kuorodheshwa kwenye listi nyeusi ya Umoja wa Mataifa ya wauaji na wanyanyasaji wa watoto. Kwa hakika, tunaweza kusema kuwa jinai ya Nuseirat ni uendeleaji wa fedheha na kashfa za kimaadili zinazouandama utawala wa Kizayuni na Marekani katika ngazi ya kimataifa.
Iran ni miongoni mwa nchi na asasi zilizolaani vikali jinai ya Nuseirat

Nukta nyingine ni kuwa, jinai ya Nuseirat kwa upande mmoja haitayafanya makundi ya Muqawama ya Palestina yaache kuendeleza mapambano na Muqawama; na kwa upande mwingine itahafifisha zaidi matumaini ya kuachiliwa huru mateka waliosalia wa Kizayuni. Abdulbari At'wan, mtaalamu mashuhuri wa Kiarabu ameandika yafuatayo kuhusiana na suala hili: "Inavyoonekana, hatua hii ya ghilba na hadaa itakuwa na matokeo hasi na mabaya; na itafuta matumaini yote yaliyokuwepo ya kuachiliwa mateka wengine 160 ambao bado wako mikononi mwa vikosi vya Muqawama vya al-Qassam na Brigedi za Quds.

 Al-At'wan amesema ana hakika kwamba mauaji ya Nuseirat hayataweza kuyafanya makundi ya Muqawama yabadilishe misimamo yao madhubuti ya kutokubali kunasa kwenye mtego wa Marekani na utawala wa Kizayuni. Wanamuqawama wa Palestina wanajua kwamba haifai kwa namna yoyote ile kukubali kuwaachilia huru mateka wa Kizayuni bila ya kutimizwa masharti yao halali na ya haki ya kutekelezwa usitishwaji vita wa kudumu, kuondoka kikamilifu majeshi ya Israel huko Ghaza na kujengwa upya eneo hilo haraka.../