Kundi la Taliban kushiriki mkutano wa Doha Qatar
Serikali inayoongozwa na kundi la wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan imetangaza rasmi nia yake ya kutuma wajumbe katika mkutano wa Doha Qatar utakaozungumzia hali ya taifa hilo.
Msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid ameziambia duru za hanari kwamba, kundi hilo linaamini ushiriki wao katika mazungumzo ya Qatar utaifaidisha linapokuja suala la msaada wa kibinaadamu na masuala ya uwekezaji.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na Umoja wa Mataifa umepangwa kufanyika tarehe 30 mwezi Juni hadi tarehe Mosi Julai.
Lengo la mkutano huo pamoja na mambo mengine ni kuongeza ushirikiano wa kimataifa na nchi hiyo inayokumbana na migogoro chungu nzima.
Tangu kurejea madarakani kwa kundi hilo mwaka 2021, kundi la Taliban limekataa miito ya kieneo na kimataifa ya kuunda serikali inayojumuisha makundi yote ya kisiasa na kuhakikisha wanawake nchini humo wanapata haki ya elimu na pia kufanya kazi. Hali hiyo imeifanya serikali ya wanamgambo wa Taliban kukabiliwa na changamoto ya kutambuliwa kimataifa.
Katika upande mwingine, fedha za nchi hiyo zimezuiliwa na mataifa ya Magharibi huku wakuu wa kundi la Taliban bado wakiwa katika orodha ya Marekani ya watu wanaotakiwa kukamatwa.