Jul 29, 2024 02:34 UTC
  • Russia: HAMAS haitatoweka, inaungwa mkono na Ulimwengu wa Kiislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema lengo la Israel la kuliondoa vuguvugu la Muqawama wa Palestina la HAMAS kazi "isiyoendana na uhalisia".

Akizungumza mwishoni mwa ziara yake nchini Malaysia baada ya kuhudhuria Mkutano wa 57 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) uliofanyika nchini Laos, Lavrov amesema Hamas haitakoma kuwapo kwa sababu inaungwa mkono na Ulimwengu wa Kiislamu.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amefafanua kwa kusema: "Israel inasema kupitia [waziri mkuu Benjamin] Netanyahu kwamba vita havitakwisha hadi Hamas itokomezwe kabisa. Kwa maoni yangu, na ya washirika wangu wengi, hiyo ni kazi isiyoendana na uhalisia".
 
Ameongezea kwa kusema: "Hamas inaendelea kuwepo na ina uwezo na uungaji mkono wa kutosha ikiwa ni pamoja na katika Ulimwengu wa Kiislamu".
Wanamuqawama wa HAMAS

Tangu Oktoba mwaka jana, Netanyahu amekuwa aking'ang'ania madai kwamba Hamas lazima "iangamizwe moja kwa moja" kabla ya Israel kukubali kumaliza vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza ikiwa tayari imeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 39,300 hadi sasa.

Kadhalika, Lavrov ametanabahisha kuwa, baadhi ya nchi zinajaribu kuandaa mapendekezo mapya ya maelewano yanayotaka kukomesha ghasia hatua kwa hatua, ikizingatiwa kuwa Israel inakataa kusitishaji mapigano mara moja.

"Baadhi ya nchi za Kiarabu, Misri na Qatar, zinafanya kazi na Wamarekani, na pia hufanya mikutano kadhaa na Waisrael", amedokeza waziri huyo wa mambo ya nje wa Russia.

Hata hivyo, amesema anahisi si vyema Wapalestina kutengwa katika mikutano inayofanywa, ikiwa hatimaye na lengo la kuamua juu ya mustakabali wao.

"Katika suala hili, tutaendelea kusaidia kurejesha umoja wa Palestina," amesisitiza Lavrov.../

Tags