Aug 06, 2024 14:11 UTC
  • Takwa la Baghdad la kuondolewa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq

Kamisheni ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraq imetoa mwito wa kuainishwa ratiba na jedwali la kuondoka wanajeshi wa Marekani kutoka katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iraq, Kamisheni ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la Iraq imekosoa kuendelea kuwepo vikosi vya kigeni nchini humo na kusisitiza ulazima wa kuandaliwa ratiba ya kuondoka askari wa kigeni kutoka Iraq. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, iwapo vikosi vamizi vitaendelea kuweko nchini Iraq, basi yamkini hali ikatoka nje ya udhibiti.

Tangu mwaka 2014, takriban wanajeshi 2,500 wa Marekani wamekuwepo nchini Iraq kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daes, na wanajeshi hao wamesambazwa katika vituo vitatu kuu: Ain al-Asad mjini Anbar, Harir mjini Erbil, na Camp Victory jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Ingawa wakati fulani waliondoka katika nchi hiyo kabla ya kundi la kigaidi la Daesh kushambulia Iraq, lakini uwepo wa Daesh ulikuwa kisingizio mwafaka cha Washington kutuma tena askari wake katika nchi hiyo ya Kiarabu. Inaelezwa  kuwa, ubalozi wa Marekani nchini Iraq ni miongoni mwa balozi kubwa zaidi za Marekani duniani, na kuwepo kwa majeshi mengi ya Washington kutoka sekta mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kiusalama na hata kijasusi kumezusha wasiwasi mwingi miongoni mwa wananchi wa Iraq. Wakati huo huo, kuendelea kuwepo kijeshi Marekani katika kambi za kijeshi nchini Iraq kwa namna fulani kunaweza kuwa ni ukiukaji wa uhuru na mamlaka ya kitaifa ya kujitawala nchi hiyo.

Ali Jamali, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Wakati serikali na Bunge la Iraq walipoitaka Marekani itoe ratiba ya kuondoka kwa majeshi yake kutoka Iraq, hii ilikuwa na maana kwamba, hawajaridhishwa na kuendelea kukaliwa kwa mabavu nchi yao. Kwa mtazamo wa Wabunge wa Iraq ni kuwa, chuki ya watu wa Iraq dhidi ya maajinabi inaweza kuwa tishio dhidi ya kuendelea kuwepo kwa majeshi ya kigeni nchini Iraq.

 

Kwa muktadha huo,  Kamisheni ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraqi inasisitiza kuwa, wawakilishi wa tume hii wamepiga kura ya kufukuzwa vikosi vya kigeni kutoka nchini humo.

Mrengo wa bunge wa Badr pia ulisisitiza kuwa vikosi vamizi vya Marekani vinapaswa kuondoka Iraq kufikia mwishoni mwa Juni ili kuepusha migogoro na vita na vikosi hivyo.

Kwa hiyo, ni wazi kabisa kwamba makundi na mirengo yote katika bunge la Iraq inataka kulindwa na kuheshimiwa ardhi yote ya nchi hiyo. Hii ni kwa sababu, endapo amani na usalama vitatawala nchini Iraq, kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini humo si tu kwamba hakutakuwa na ulazima wowote na uhalalishaji bali kunaweza pia kuchochea hisia za kupigania mamlaka ya kujitawala za wananchi wa nchi hiyo.

Bunge la Iraq

 

Katika mazingiara haya, moja ya masuala yanayofuatiliwa na bunge la Iraq ni kukata mikono ya Wamarekani katika uchumi wa Iraq na sekta ya mafuta. Ingawa Marekani inajifanya kuwa haihusiki katika masuala ya kisiasa ya Iraq, lakini kwa kuchukua mkondo wa masuala ya fedha na mafuta ya Iraq, Washington kwa hakika inaathiri uchumi na mamlaka ya kitaifa ya Iraq. Kiasi kwamba, serikali ya Iraq inahitaji kupata idhini ya Hazina na Benki Kuu ya Marekani kwa ajili ya kujidhaminia mahitaji yake ya kifedha.

Suala hilo linachukuliwa na weledi wa mambo na vyama vya siasa vya Iraq kuwa ni udhalilishaji. Kwa msingi huo, inawezekana kusema kuwa, juhudi za Kamisheni ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraq za kuwaondoa wageni kutoka nchi humo ni kukataa mikono ya Marekani katika masuala mbalimbali ya kijeshi, kiuchumi, kifedha na mafuta ya Iraq.

Wakati Baghdad inasisitiza juu ya ulazima wa kuhitimishwa operesheni za muungano wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, ni jambo lililo mbali katika mazingira ya sasa ambapo Marekani inajiandaa na uchaguzi wa Rais kuiona ikikubali kutia saini makubaliano ya kuondoka kwa vikosi vyake kutoka Iraq.