Wazayuni wazidi "kumkalia kooni" nduli wa Ghaza
Matokeo ya uchunguzi wa karibuni kabisa wa maoni uliofanywa na Kanali ya 12 ya televisheni ya Israel yanaonesha kuwa, walowezi wengi wa Kizayuni wanaoishi katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, wanachukizwa sana na kuendelea Benjamin Netanyahu kung'ang'ania kuwa waziri mkuu wa utawala huo.
Shirika la habari la FARS limeinukuu televisheni hiyo ya utawala wa Kizayuni ikisema kuwa asilimia 69 ya walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wanapinga kuendelea Benjamin Netanyahu kuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni huku asilimia 22 ikitaka aendelee kubakia madarakani hadi wakati wa uchaguzi mpya.
Waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni, Naftali Bennett hivi karibuni aliashiria kuongezeka ukosefu wa amani ndani ya safu za Wazayuni na kukiri kwamba siasa za Netanyahu zimepelekea kila siku Wazayuni wengi wakimbie ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.
Familia za mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa wanamapambano wa Palestina pia zinasema kuwa, Netanyahu ndiye kikwazo na mkosa mkuu wa kushindwa kuachiliwa huru jamaa zao kutoka mikononi mwa HAMAS na wameonya kuwa kama Netanyahu ataendelea kukwamisha mazungumzo, basi moto wa vita utaenea katika eneo zima la Asia Magharibi.
Walowezi wa Kizayuni wanaoishi katika vitongoji vilivyojengwa na utawala wa Kizayuni nao kwa miezi mingi sasa wanaendesha maandamano makubwa ya kupinga serikali ya Netanyahu na wanashinikiza vita vya Ghaza vikomeshwe ili ipatikane fursa ya kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni.